Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA ya mwaka 2015, zaidi ya nchi 30 duniani, theluthi moja zikitoka Afrika zinajiandaa kuanzisha mipango ya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa usaidizi wa wataalamu kutoka Urusi.

Miaka ya hivi karibuni katika kuidhinisha matumizi ya nishati ya nyuklia, Kampuni ya Urusi Rosatom, tayari imeshaingia makubaliano na baadhi ya nchi za Afrika na miongoni mwao ni Rwanda.

Mwaka jana kampuni hiyo ilitangaza kwamba imesaini makubaliano (MOU) na serikali ya Rwanda kupitia wizara yake ya miundo mbinu kushirikiana katika matumizi ya amani ya nishati ya atomiki.

Makubaliano hayo yaliidhinishwa kwa misingi ya ushirikiano wa pande mbili kujenga miundo mbinu ya nyuklia Rwanda na miradi mingine inayotokana na teknolojia ya nyuklia kama ilivyo kwa Uganda hivi sasa katika sekta zikiwemo za afya na hata ukulima.

Rwanda inasema teknolojia ya nyuklia itaifaa kwa matumizi ya kutengeneza nishati, dawa na matumizi mengine ya amani lakini imepingwa vikali na upande wa upinzani nchini humo.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Green nchini Rwanda, Frank Habineza amepinga mpango wa nchi yake kujenga kiwanda cha nyuklia kwa ushirikiano na Urusi akisema utakuwa na athari mbaya kwa wananchi.

Akizungumza na BBC, Habineza amesema wao hawakuunga mkono ushirikiano huo baina ya serikali ya Rwanda na Urusi kutokana na athari zake.

“Kulikuwa na mapatano ya Vienna kuhusu maswala ya nyuklia, na wakati huo huo Rwanda ilisaini mapatano mengine na Urusi kuanzisha kiwanda cha nyuklia hapa Rwanda. Mapatano ya Vienna yalikuwa kama kupalilia njia ya hayo ya Urusi kuanza kutekelezwa.” Amesema Habineza.

Kiongozi huyo wa upinzani ametaja mfano wa nchi ya Ukraine ambako kiwanda cha nyuklia kililipuka na kuathiri nchi jirani ya Sweden.

Muswada huo wa ujenzi wa nguvu za nyuklia ulipitishwa bungeni Rwanda isipokuwa pingamizi ya wabunge wawili tu ambao hawakuunga mkono.

Kenya, Afrika kusini na Nigeria ni miongoni mwa mataifa mengine ya Afrika yalio na ushirikiano na Urusi katika kuidhinisha miradi ya matumizi ya nishati ya nyuklia.

Video: Aliyetoka jela kwa msamaha aunda kikosi cha wizi wa Bodaboda
Serikali yasifu juhudi za ALAT