Wakali wa sauti na melodi kutoka Kenya na Tanzania wamekutana kwenye ngoma moja waliyoiita ‘Nishikilie’, ambapo leo wameachia video yake.

Willy Paul ameiwakilisha Kenya akitokea Saldido International wakati Ali Kiba na Ommy Dimpoz wa Rockstar Africa wakiiwakilisha ardhi ya Mwalimu Nyerere, Tanzania.

‘Nishikilie’ ni wimbo uliopikwa  na mtayarishaji Teddy ambaye anafanya kazi na Saldido International. Ndani ya ngoma hiyo, wakali hao wa ‘malavidavi’ kila mmoja anamsifia msichana wake wa kiafrika mwenye mahaba kutoka Pwani ya Afrika Mashariki.

Video ya ngoma hiyo iliyoongozwa na Ivan, imepokelewa vizuri YouTube. Ndani ya saa chache, imetazamwa zaidi ya mara 59,000. Hii ni moja kati ya video ya muziki ambayo inaweza kuvuta watazamaji milioni ndani ya saa 24. Tusubiri…!

Willy Paul amefungua kwa melodi za kumlaza Simba wa Mikumi, Ommy Dimpoz akaingia katikati akileta ladha tofauti na sauti laini iliyofuatiwa na ile tuliyoizoea kutoka kwa mkali huyo wa ‘You are the Best’, kabla ya King Kiba kufunika na kiitikio kinachokuamsha kwenye kiti… akimaliza na mchanganyiko wa vibwagizo vinavyosindikizwa na Mkenya Willy Paul.

Video ya ‘Nishikilie’ imeshambuliwa vizuri na ‘dancers’ wakiongozwa na Willy Paul pamoja na manjonjo ya wana Rockstar Africa.

Angalia video hapa:

RC Makonda aonya kuhusu Coco Beach, 'Hii hujuma haikubaliki'
Manara atuma ujumbe kwa wana Simba kuhusu Yanga Vs Township Rollers