Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuenzi misingi ya utawala bora haitamvumilia kiongozi yeyote wa umma atakayekiuka misingi hiyo na kutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya umma katika utendaji wake.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika Kitaifa jijini Dodoma, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaasa viongozi wote kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utendaji wao kwani hiyo ndio njia pekee itakayoepusha mgongano wa maslahi.

Majaliwa amesema mgongano wa maslahi umechangia rasilimali za nchi kunufaisha watu wachache huku wananchi wengi kuendelea kuwa fukara, wakati wachache wakijitajirisha isivyo halali, hivyo Serikali itaendelea kuziba mianya, kwani ikiachiwa iendelee, itarudisha nyuma jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Pia ameeleza kuwa mmomonyoko wa maadili umechangia sana kutozingatiwa kwa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali katika utumishi wa umma, tatizo ambalo limesababisha mgongano wa maslahi.

Amesema mgongano wa maslahi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuisababishia hasara Serikali kwa muda mrefu, tatizo ambalo lazima lidhibitiwe kwani mara kadhaa baadhi ya viongozi au watumishi wa umma wamekuwa wakifanya maamuzi kwa mambo wanayojua wazi kuwa wana maslahi binafsi nayo.

”Mathalan katika Halmashauri zetu wapo madiwani au watumishi wanaoshiriki kutoa maamuzi yanayohitimishwa kwa kumpatia kazi mkandarasi au mzabuni wakati kampuni husika inamilikiwa na mwenza, rafiki, ndugu wa karibu au mtoa rushwa.”

Majaliwa ameongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kuunga mkono na kutekeleza Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa ipasavyo. Mikataba hiyo ni pamoja na mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa na Makubaliano yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu.

”Sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi katika ibara ya 145 (a), ambapo tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mojawapo ya agenda yetu ilikuwa ni kuendeleza jitihada za kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na utawala wa sheria katika ngazi zote za uongozi.

Ole Nasha atoa neno Simanjiro, asisitiza ushirikiano
Kagasheki ang'aka, aitaka TRA kutekeleza maagizo ya JPM