Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ndio yenye jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo na kwamba taarifa zinazosambazwa za kuwepo kwa baa la njaa nchini hazina ukweli wowote na Serikali inawahakikishia wananchi kuwepo kwa usalama wa chakula, hivyo amewataka Watanzania kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani si za kweli bali ni za uzushi zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.

Majaliwa amesema hayo Januari 16, 2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa mara baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, ambapo amesisitiza kwamba hali ya upatikanaji chakula nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Waziri Mkuu amesema hayo baada ya kutolewa kwa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu kuwepo kwa baa la njaa nchini jambo ambalo si la kweli. Amewataka wananchi kuwa watulivu na jambo hilo likitokea Serikali itatoa taarifa.

“Naomba wananchi msiwe na wasiwasi juu ya hali ya chakula nchini. Msisikilize kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja kwenye baadhi ya vyombo vya habari yakiwemo magazeti kwani taarifa hizo si za kweli. Chakula kipo cha kutosha licha ya mvua kusuasua katika baadhi ya maeneo nchini,” – Majaliwa.

Mbarawa azitaka taasisi kujiunga na kituo cha kumbukumbu IDC
Nape atoa neno kuhusu TBC