Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa haitavumilia wakandarasi wasio na uwezo na ambao wanapewa kazi lakini wanashindwa kuzimaliza katika muda uliopangwa.

Hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi wa mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhia maji Chalinze unaimarika na kufikia asilimia 80 la sivyo, wakamilishe taratibu za kukatisha mkataba na kutafuta mkandarasi mwingine.

“Nimeelezwa kwamba mmempatia nyongeza ya siku 100 ambayo inaisha tarehe 31 Mei 2017, kama kazi yake haitakuwa ya kuridhisha na kufikia walau asilimia 80, itabidi Waziri uendelee na taratibu zako za kukatisha mkataba, tuanze kutafuta mkandarasi mwingine,” amesema Majaliwa.

Agizo hilo ni kufuatia taarifa aliyopewa kwamba mkandarasi wa mradi huo, Overseas Infrastructure Alliance (OIA) Pvt Ltd ya India alipaswa kumaliza kazi hiyo Februari 22, mwaka huu lakini hadi sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 23 tu.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Halmamshauri ya Chalinze na wale wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (CHALIWASA) katika ofisi zao, karibu na daraja la mto Wami, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Majaliwa ameenda Chalinze kukagua mradi huo ambao umechukua muda mrefu lakini haujakamilika. Awamu ya kwanza ulianza mwaka Septemba mosi 2001 na kukamilika Desemba mosi 2003.

Aidha, Majaliwa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa CHALIWASA, Eng. Christer Mchomba, ahakikishe kuwa wanapeleka maji hadi majumbani mwa wateja na kuweka mita ili wananchi waweze kulipa bili zao badala kuishia kutoa huduma hiyo kwenye vioski (viula).

 

 

 

Uwanja Wa Namfua Waonesha Dalili za Mawingu Ya Mvua ya Ligi Kuu
Mbappe Ataka Aachwe Avute Pumzi, Amezewa Mate na Wababe