Mbunge wa Jimbo la Busega kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Raphael Chegeni amewataka makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdrlahaman Kinana na Yusuf Makamba kuacha kuingiza misuguano ndani ya chama na serikali.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa waraka ulioandikwa na wastaafu hao na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari wakitoa malalamiko kuhusu kitendo cha Cyprian Musiba kuwasema hadharani si cha kiungwana.

Amesema viongozi hao hawakupaswa kusambaza waraka huo kwenye mitandao ya kijamii kwani kufanya hivyo, ni kwenda kinyume cha katiba ya chama cha mapinduzi, ambapo amesema kuwa walitakiwa kupeleka malalamiko yao katika kamati ya maadili.

Aidha, ameongeza kuwa viongozi hao wastaafu tayari walishafanya mambo makubwa zaidi katika nchi hii, hivyo wanaelewa taratibu zote ambazo walitakiwa kuzifuata.

”Kwakweli siridhishwi na kile kinachoendelea, hawa viongozi wetu wastaafu walishafanya mambo makubwa sana katika kipindi chao, sasa kwa hili hawakupaswa kukimbilia kwenye mitandao na vyombo vya habari kumlalamikia Musiba ambaye anajiita mwanaharakati huru, kwani vyombo vya sheria vipo, wamevunja katiba ya CCM,”amesema Dkt. Chegeni

Hata hivyo, hivi karibuni, viongozi hao wastaafu wa chama cha mapinduzi (CCM) waliandika waraka wakilalamika kuhusu Cyprian Musiba kuwataja katika tuhuma mbalimbali bila kuchukuliwa hatua zozote.

Waziri Mkuu azindua zoezi la Uboreshaji Daftari la Wapiga Kura
Iwe Mvua au Jua, Rais Magufuli ni mgombea wetu CCM 2020- Bashe