Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Aprili 24, 2019 ameondoka nchini Tanzania na kwenda nchini Malawi ambako anafanya ziara rasmi ya Kiserikali ya siku 2 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Prof. Arthur Peter Mutharika.

Akiwa ziarani Malawi, pamoja na Mambo mengine yote lakini pia ziara hiyo ina lengo la kuimarisha umoja na mshikamano katika nyanja mbali mbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Rais Magufuli akiwa na Mkewe, Mama Janeth Magufuli ameondoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo amepokelewa rasmi na mwenyeji wake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu Mjini Lilongwe.

Akiwa Mjini Lilongwe Rais Magufuli ataweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya aliyekuwa Rais wa Malawi Hayati Bingu Mutharika, kisha atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Mutharika, na jioni atahudhuria Dhifa ya Kitaifa aliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais Mutharika.

Aidha, hapo kesho Rais Magufuli akiwa na mwenyeji wake Rais Mutharika atamaliza ziara yake kwa kufungua msimu wa soko la Tumbaku na kuzungumza na wadau wa zao hilo na baadaye atarejea nchini Tanzania ambako ataanza ziara ya kikazi ya siku 8 katika mkoa wa Mbeya.

Serikali kuweka bei elekezi ya Pembejeo za kilimo
Kundi la ISIS limetangaza kuhusika na Mashambulizi ya Sri Lanka