Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametoa siku kumi kwa wafanyabiashara wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi kujisalimisha mara moja ili waweze kueleza ni wapi wanako zipitishia kuziingiza Jijini Dar es salaam.

Ameyasema hayo mapema hii leo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wasanii wa Maigizo Maarufu kwa jina la ‘Bongo Movie’ walipomtembelea Ofisini kwake na kutoa malalamiko yao kuhusu kazi zao zinavyoibiwa na kutothaminiwa na wafanyabiashara hao.

Amesema kuwa anatoa siku kumi kwa wafanyabiashara hao kujisalimisha wao wenyewe na kueleza wanakozipitishia kuziingiza Jijini Dar es salaam.

“Haiwezekani watu wanaleta biashara zao kutoka nje ya nchi lakini haieleweki zinapoingilia lakini unakuta mtaani zimejaa kila kona, wakati Rais Dkt. Magufuli anataka kila mfanyabiashara anatakiwa alipe kodi,” amesema Makonda.

Aidha, katika hatua nyingine amesema kuwa bidhaa zinazozalishwa na wasanii zinatakiwa kuheshimiwa na ameahidi kuungana nao ili kuweza kuhakikisha wanapata haki zao za msingi kwani kazi wanayoifanya ni kubwa.

Hata hivyo, amesema kuwa tayari ameshawasiliana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na kuwasilisha matatizo yao ili yaweze kufanyiwa kazi.

Magazeti ya Tanzania leo Aprili 9, 2017
Serikali ya Morocco kukabiliana na athari ya mabadiliko ya Tabianchi