Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemkabidhi Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya wilaya ya Rorya, Mhandisi Obetto Sasi kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Majaliwa ametoa uamuzi huo Januari 16, 2018 wakati aliposimamishwa na umati wa wananchi kwenye mji Mdogo wa Shirati alipokuwa njiani kuelekea kwenye kijiji cha Bubombi wilayani Rorya.

“Hatuwezi kuwa na mtumishi wa aina hii ambaye kila eneo tunakutana na changamoto za maji huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya Serikali kutoa fedha, hivyo namuagiza Katibu Tawala wa Mkoa alete mhandisi mwingine wa maji.”

Pia, Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Profesa Kitila Mkumbo kwenda wilayani Rorya na kukagua mradi wa maji katika mji Mdogo wa Shirati na kuona namna ya kuutekeleza.

Amesema kwa sasa Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo. Kampeni hiyo  inalenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo itawachukulia hatua wote watakaokwamisha miradi ya maji.

Wilaya ya Rorya inatekeleza miradi 11 ya maji ya bomba kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RWSSP) katika vijiji vya Kinesi, Randa, Utegi, Mika,Kirogo, Nyihara, Kisumwa,Nyamkonge, Nyambori, Gabimori na Marasibora.

Kingwangalla: Wasichana warembo na wakaka watanashati kuajiriwa
Yanga yasaini dili nono