Mtangazaji maarufu wa Clouds FM, Adam Mchomvu amefunguka ushauri wake kwa bosi wa WCB, Diamond Platinumz kuhusu uhusiano wake na vyombo vingi vya habari.

Mchomvu amefunguka Aprili 3, 2019 alipofanya mahojiano maalum na The Playlist ya Times FM, ambapo amedai kuwa mkali huyo wa ‘Tetema’ anaweza kufika mbali zaidi endapo atatulia na kuacha kuvimba dhidi ya vyombo vya habari.

“Ni mtu ambaye amefanikiwa sana kwenye hii game ya muziki, yaani imemuotesha mabawa yuko pale juu anafly (anapaa). Sasa sijui ni kitu cha kuiga au ni kitu cha kujifunza au nini mimi mwenyewe sijajua bado,” aliiambia The Playlist.

“Mtu anaweza kuwa na confidence (kujiamini) kwa kiasi hicho, kwamba hujali kuhusu media..! Wewe unafanya muziki ni vitu ambavyo mnahusiana. Kwahiyo mimi namshauri tu a-calm down (atulie) dogo yuko vizuri anafanya vizuri, yaani akituliza wenge anaweza akawa vizuri zaidi. Pamoja kwamba ana redio, ana TV, jina kubwa, wafuasi wengi. Dunia nzima wanamjua sasa hivi, atulie tu kuliko kuvimbiana-vimbiana na media sijui nani, sio fresh sio poa,” aliongeza.

Nyimbo za Diamond hazipigwi na vituo kadhaa vya redio ikiwa ni pamoja na Clouds Media Group pamoja East Africa Radio/TV. Diamond amewahi kueleza kuwa kwa sasa hategemei redia na televisheni kuuza muziki wake, kwani hata mitandao yake ya kijamii ikiwa ni pamoja na YouTube vinaweza kumsogeza zaidi.

Katika hatua nyingine, Mchomvu ambaye alienda katika kituo hicho kwa lengo la kutambulisha wimbo wake mpya ‘A.D.A.M’, alipiga kura yake akimchagua Ali Kiba dhidi ya Diamond, baada ya mtangazaji wa kipindi hicho, Lil Ommy kumtaka amchague mmoja kati yao ambaye angempa tuzo ya msanii bora wa RnB/Bongo Fleva endapo angetakiwa kufanya hivyo wakati huu.

Alisema ingawa Diamond ni rafiki yake, yeye ameamua ampe Ali Kiba kutokana na ubora wa sauti yake.

“Ali Kiba si ni mnyama kabisa. Sauti ile, uimbaji mzuri, discipline (nidhamu), focus. Nampa Ali Kiba… Diamond ni mwanangu lakini hii nampa Ali Kiba,” alisema Mchomvu.

Mchomvu pia alitupa karata yake nyingine alipoambiwa kuchagua kati ya Nikki wa Pili na Nikki Mbishi, ambapo alimchagua Nikki Mbishi kutoka Tamaduni Music ingawa alisema kuwa tatizo lake ni ‘ubishi tu’.

Jokate afunguka mafanikio kampeni ya tokomeza zero, mamilioni yakusanywa
LIVE: Ziara ya Rais Magufuli mkoani Ruvuma