Klabu ya Real Madrid imemteua kocha wa sasa wa timu ya taifa ya Hispania, Julen Lopetegui kuwa kocha mpya wa klabu hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu.

Julen Lopetegui anakwenda Santiago Bernabeu kurithi mikoba ya Zinedine Zidane ambaye ameipatia Real Madrid mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na kushinda mataji matatu ya klabu bingwa kabla ya kutangaza kujiuzulu kuifundisha klabu hiyo mwezi Mei.

Mwaka 2003 Lopetegui alianza kazi ya ukocha kama kocha msaidizi wa timu ya Hispania chini ya miaka 17 na baadae akawa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania chini ya miaka 19, 20 na 21. Kocha huyo pia aliwahi kuwa kocha wa klabu ya FC Porto kwa miaka miwili kabla ya kuchukua uongozi wa timu ya taifa ya Hispania ya wakubwa mwezi Julai mwaka 2016.

Tangu amekuwa kocha wa timu ya taifa Hispania haijafungwa, ikiwa imeshinda michezo 14  na kupata droo sita katika mechi 20. Rekodi yake katika timu ya taifa sio mbaya mpaka sasa lakini linapo kuja swala la majukumu ya kuwa kocha wa Real Madrid ndipo swali linapokuja kwamba je ataweza kufanya makubwa aliyofanya Zidane na kumridhisha Florentino Perez?.

Tusubiri kuona atakachokifanya kocha huyo mwenye umri wa miaka 51 kwani ataanza rasmi kibarua chake baada ya kombe la dunia ambalo linaanza tarehe 14 Juni.

Video: Nape akubali lawama ya 'Bao la mkono', JPM awapasha viongozi wa dini
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 13, 2018

Comments

comments