Viongozi wa chama cha soka nchini Urusi RFU, wametakiwa kulikemea vikali suala la ubaguzi wa rangi ambalo linaonekana kushika kasi nchini humo.

Ushauri kwa viongozi wa RFU umetolewa na umoja wa waandishi wa habari nchini Uingereza kwa kuwataka viongozi wa soka nchini humo kuangalia umuhimu wa jambo hilo ambalo huenda likaharibu mipango ya maandalizi ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

Msukumo wa ushauri huo kwa viongozi wa RFU, umetokana na tukio lililojitokeza mwishoni mwa juma lililopita, pale kiungo kutoka nchini Uingereza, Emmanuel Yaw Frimpong alipokumbana na madhila ya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa klabu ya Spartak Moscow wakati wa mchezo wa ligi nchini humo.

Frimpong ambaye anaitumikia FC Ufa, alikerwa na kelele mashabiki wa klabu ya Spartak Moscow, zilizokua zikiigiza mlio wa nyani ambazo zilisikika kila alipokua akimiliki mpira na hatimae aliwageukia wahusika na kuwaonyesha kidole cha kati.

Hata hivyo kitendo cha kuwanyooshea kidole cha kati mashabiki hao, kilimsababishia kiungo huyo ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Arsenal, kuadhibiwa kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.

Inahofiwa huenda vitendo vya kibaguzi vikaendelea kukomaa nchini Urusi, hali ambayo huenda ikawa karaha kwa baadhi ya timu zenye wachezaji wenye asili ya Afrika wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.

 

Nyota Ya Uingereza Yamuwakia Abou Diaby Wa Arsenal
Kagame Cup Yaivuruga Yanga