Leo tunalifunga kundi G lenye timu za Ubelgiji, Panama, Tunisia na Uingereza (England).

England ni taifa kubwa sana katika ramani ya soka duniani, na mashabiki wengi waliitarajia kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka huu kutokana na kuwa na wachezaji mashuhuri.

Taifa hilo linaloongozwa chini ya utawala wa Malkia Elizabert, lilifuzu fainali za mwaka huu likitoke ukanda wa barani Ulaya (UEFA), kwa kufanikiwa kuongoza msimamo wa kundi F (Kundi La Sita), lililokuwa na timu za mataifa ya Slovakia, Scotland, Slovenia, Lithuania na Malta.

England iliongoza msimamo wa kundi hilo kwa kufikisha alama 26, zilizotokana na ushindi katika michezo minane, kutoka sare mara mbili na hawakupoteza mchezo.

Kanuni za kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia kupitia ukanda wa bara la Ulaya (UEFA) za kuitaka timu iliyoongoza msimamo wa kundi kushiriki moja kwa moja, ziliiwezesha England kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokwenda Urusi.

Jina la utani la timu ya taifa ya England: The Three Lions.

Mfumo: Kikosi cha England hutumia mfumo wa 3-4-2-1.

Image result for Harry Kane - englandMchezaji Nyota na Nahodha: Harry Kane (Tottenham Hotspur)

Image result for Marcus Rashford - englandMchezaji hatari: Marcus Rashford (Manchester United)

Image result for Gareth Southgate - englandKocha: Gareth Southgate (47), raia wa England.

Ushiriki: England imeshiriki fainali za kombe la dunia mara kumi na nne (14). Mwaka 1950, 1954, 1958, 1962, 1966, 1970, 1982, 1986, 1990, 1998, 2002, 2006, 2010 na 2014.

Mafanikio: Mabingwa (1966)

 

Kuelekea 2018:

Kikosi cha England kilifuzu kwa namna yake, chini ya kocha Gareth Southgate ambaye alikuwa haaminiwi sana na mashabiki wa soka nchini humo kutokana na uzoefu aliokuwa nao hasa baada ya uteuzi wake kufuatia kuondolewa kocha Sam Allardyce.

Kabla ya kutangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya England Southgate alikabidhiwa jukumu la kuwa kocha wa muda wa timu hiyo, akitokea kwenye kikosi cha chini ya umri wa miaka 21.

Hata , baadhi ya mashabiki wa soka nchini England walionesha kutokuwa na imani kwa kocha huyo, wakati wa fainali za mataifa ya Ulaya za mwaka 2016 zilizochezwa nchini Ufaransa, kufuatia kikosi chake kufika hatua ya mtoano (16 Bora), na kutolewa na Iceland.

England imekuwa na matokeo mazuri ya kutopoteza mchezo wowote wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia tangu Oktoba 2009. Kwa jumla wamecheza michezo 39, chini a utawala wa makocha watatu tofauti.

Gareth Southgate hakutaka kubadilisha mfumo wa kikosi cha England, aliendelea na utamaduni wa kukipanga kikosi chake kwa kuzingatia mfumo wa 3-4-2-1 ambao ulikuwa chachu ya kupata mafanikio ya kufuzu.

England wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Tunisia, Uwanja wa Volgograd mjini Volgograd Juni 18, kisha watapambana na Panama Juni 23, Uwanja wa Nizhny Novgorod mjini Novgorod, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Ubelgiji Juni 28, uwanja wa Kaliningrad mjini Kaliningrad.

Leo tumefunga kundi G, kesho tunaanza kundi la mwisho, Kundi H kabla hatujaingia ndani ya mashindano ya fainali za kombe la dunia. Kaa nasi hapa, Dar24 Media na tembelea YouTube Channel yetu kupata mengi zaidi. Tunakupeleka Urusi na kukuchambulia yanayojili.

UDSM yapata pigo, wanafunzi watatu wafariki dunia
Magazeti ya Tanzania leo Juni 12, 2018