Bila shaka unajiandaa kwa kuanza kufuatilia mshike mshike wa fainali za kombe la dunia ambazo zitaanza wakati wowote kuanzia sasa baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

Dar24 leo tunakukamilishia makala za uchambizi wa timu shiriki katika fainali za kombe la dunia za mwaka huu kwa kuimulika timu ya taifa ya Japan, ambayo imapangwa katika kundi H, lenye timu za Poland, Senegal na Colombia.

Japan ililazimika kupambana vilivyo kuwania nafasi ya kushiriki fainali kombe la dunia, kutokana na mlolongo mrefu wa ushiriki wa ukanda wa barani Asia (AFC) ambapo mataifa mengi hushiriki katika hatua za awali.

Japan ilianza kupambana katika mzunguuko wa pili wa kuwania kufuzu fainali hizo ikipangwa katika kundi E (Kundi La Tano) lililokua na timu za mataifa ya Syria, Singapore, Afghanstan na Cambodia.

Taifa hilo la mashariki ya mbali lilifanya vyema kwenye michezo ya kundi hilo na lilifanikiwa kuongoza msimamo kwa kufikisha alama 22, zilizotokana na ushindi wa michezo saba na kutoka sare mchezo mmoja, huku likigoma kufungwa.

Japan wakaendelea katika mzunguuko wa nne wa kuwania kufuzu kupitia ukanda wa barani Asia (AFC), na walipangwa katika makundi kwa mara nyingine tena, safari hii waliangukia kwenye kundi B (Kundi La Pili), lililokua na timu za mataifa ya Saudi Arabia, Australia, United Arab Emirates (UAE), Iraq na Thailand.

Kutokana na ubora wa kikosi cha Japan, mambo yaliendelea kuwa mazuri upande wao, kutokana na kumaliza michezo ya kundi hilo na kuongoza msimamo kwa kufikisha alama 20, zilizotokana na ushindi wa michezo 6, sare mara mbili na walipoteza michezo miwili.

Kwa mafanikio hayo Japan ilijipatia tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2018.

Jina la utani la timu ya taifa ya Japan: Samurai Blue

Mfumo: Kikosi cha Japan hutumia mfumo wa 4-3-3.

Image result for Maya Yoshida - japanMchezaji Nyota: Maya Yoshida (Southampton)

Image result for Yosuke Ideguchi - japanMchezaji hatari: Yosuke Ideguchi (Gamba Osaka)

Image result for Makoto Hasebe - japanNahodha: Makoto Hasebe (Eintracht Frankfurt)

Image result for Akira Nishino - japanKocha: Akira Nishino (63), raia wa Japan.

Ushiriki: Japan imeshiriki fainali za kombe la dunia mara tano (05). Mwaka 1998, 2002, 2006, 2010 na 2014

Mafanikio: Hatua ya 16 Bora (2002, 2010)

Kuelekea 2018:

Japan wamekua kivutoa kikubwa katika ushiriki wa fainali za kombe la dunia, kutokana na kuwa na utamaduni wa soka la tofauti na mataifa mengine shiriki.

Tangu walipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1998, Japan wameonyesha soka la kupambana na kila taifa duniani bila kuhofia ukubwa wa jina ama umaarufu wa wachezaji wa timu wanayocheza nayo.

Hali hiyo huifanya timu ya taifa hilo la mashariki ya mbali lenye watu zaidi ya 126,672,000 kuonyesha soka lenye ushindani, japo limekua halina bahati ya kufika mbali.

Mwaka huu Japan wanatarajiwa kuwa moja ya mataifa yatakayo onyesha soka lenye ushindani zaidi kutokana na kuwa na mwenendo mzuri tangu walipokua wakisaka nafasi ya kushiriki fainali za 2018.

Waliongoza kila kundi walilopangwa kwa kuzichapa timu pinzani, hali ambayo inamaanisha wana kikosi kizuri ambacho kitakua na muendelezo wa kaliba yao ya kupambana bila kuchoka.

Wachezaji wenye uzoefu kama Shinji Okazaki, Shinji Kagawa, Hiroki Sakai, Gotoku Sakai, Gen Shoji, Naomichi Ueda, Yuya Osako, Yoshinori Mutona  Takuma Asano, wanatazamiwa kuongeza chachu kwa wachezaji chipukizi Genki Haraguchi, Takashi Usami (Fortuna Dusseldorf); Gaku Shibasaki (Getafe), Ryota Oshima (Kawasaki Frontale), Kento Misao (Kashima Antlers), Yosuke Ideguchi (Leonesa) Masaaki Higashiguchi (Gamba Osaka) na Kosuke Nakamura (Kashiwa Reysol) ambao watakua wakishiriki kwa mara ya kwanza fainali za mwaka huu.

Japan wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Colombia, Uwanja wa Mordovia mjini SaranskJuni 19, kisha watapambana na Senegal Juni 24, Uwanja wa Central mjini Yekaterinburg, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Poland Juni 28,uwanja wa  Volgograd mjini Volgograd

Kuwa na utazamaji/ufuatiliaji mwema wa michezo ya fainali za kombe la dunia mwaka huu 2018, endelea kuifuatilia kwa karibu Dar24 kwenye tovuti, mitandao ya kijamii na YouTube ambayo ni Dar24 Media ili uendelee kuwa karibu na Urusi mwaka huu.

Jamii Forums yawatahadharisha wateja wake
Serikali yatoboa siri elimu bure hadi chuo kikuu