Wakati joto la kukanyaga nyasi za viwanja vya soka vilivyoandaliwa kwa kiwango cha kisasa nchini Urusi, moja ya mataifa yenye nguvu kubwa duniani, tunaendelea kuzimulika kwa ufupi timu zinazoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, na leo tunaimulika Australia iliyopangwa kundi C.

Timu za kundi hili ni Ufaransa, Australia, Peru na Denmark.

Australia ilikuwa timu ya 31 kufuzu fainali za kombe la dunia 2018, tena katika mazingira magumu ya kusafiri umbali mrefu kuliko timu yoyote iliyocheza hatua za kufuzu.

Australia walisafiri umbali wa kilomita 250,000 kuwafuata wapinzani wao kama Saudi Arabia, Bangladesh, Tajikistan, Iran, Japan, Malaysia na Honduras.

Taifa hili lilicheza michezo ya kufuzu kupitia ukanda wa bara la Asia na lilimaliza michezo ya kundi B (Kundi La Pili) katika nafasi ya tatu kwa kukusanya alama 19, nyuma ya Saudi Arabia waliomaliza kwenye nafasi ya pili kwa alama 19 lakini walifaulu kwa kucheza mchezo wa mtoano, kwani walikuwa na uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kundi hilo liliongozwa na Japan, waliojikusanyia alama 20 na kufuzu moja kwa moja.

Australia walilazimika kusubiri mchezo wa mtoano dhidi ya mshindi wa tatu wa kundi A ambaye alikuwa Syria na walifanikiwa kushinda jumla ya mabao matatu kwa mawili, baada ya kucheza michezo ya nyumbani na ugenini.

Mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Hang Jebat Stadium, Krubong (Malaysia),  Australia walilazimisha sare ya bao moja kwa moja, na mchezo wa mkondo wa pili uliochezwa Stadium Australia, Sydney, wenyeji Australia walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Ushindi huo haukutosha kuipeleka Australia kwenye fainali za kombe la dunia, kwani iliwalazimu kuwasubiri Honduras waliomaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa kundi la Amerika ya kusini.

Mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu kwa wawili hao ulichezwa Estadio Olímpico Metropolitano, San Pedro Sula, na timu hizo kwenda sare ya bila kufungana, huku mchezo wa pili uliounguruma Stadium Australia, Sydney, ulishuhudia Australia wakitakata kwa ushindi wa mabao matatu kwa moja.

Jina la utani la timu ya taifa ya Australia: Socceroos

Mfumo: Kikosi cha Australia hutumia mfumo wa 3-4-1-2.

Image result for Aaron MooyMchezaji Nyota: Aaron Mooy (Huddersfield Town) .

Image result for Mathew LeckieMchezaji hatari: Mathew Leckie (Hertha Berlin).

Related imageNahodha: Michael John “Mile” Jedinak (Aston Villa).

Image result for Lambertus "Bert" van MarwijkKocha: Lambertus “Bert” van Marwijk (65), raia wa Uholanzi.

Ushiriki: Australia imeshiriki fainali za kombe la dunia mara nne (4). Mwaka 1974, 2006, 2010 na 2014.

Mafanikio: Kufika hatua ya mtoano (16 bora-2010).

Kuelekea 2018:

Kocha Lambertus “Bert” van Marwijk atakuwa na kazi kubwa ya kuuhakikishia umma wa soka duniani, kuwa anaweza kufanikisha harakati za kuifikisha mbali Australia, hasa baada ya kukabidhiwa jukumu hilo Januari 24 mwaka 2018, akichukua nafasi ya kocha Graham Arnold, ambaye alifanikisha safari ya Socceroos ya kuelekea Urusi.

Kikosi cha Australia bado kinamtegemea sana mkongwe Tim Cahill ambaye amefikisha umri wa miaka 38.

Wengine wanaotegemewa kwenye kikosi cha Socceroosni Aaron Mooy, Tom Rogic na Massimo Luongo.

Australia itaanza kampeni za kuusaka ubingwa mwaka huu kwa kucheza dhidi ya Ufaransa, Uwanja wa Kazan, mjini Kazan Juni 16, kisha watapambana na Denmark Juni 21, Uwanja wa Cosmos Arena, mjini Samara, na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi watakutana na Peru Juni 26, Uwanja Fisht Olympic, mjini Sochi.

Hii ni Australia, wenye historia ambayo sio nzuri sana kwenye fainali hizi za Kombe la Dunia, je mwaka huu wataisafisha historia yao katikati ya msitu wa kundi C? Tusubiri sauti ya kipyenga.

Endelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi fupi hapa hapa Dar24, kesho tutaimulika timu nyingine ya kundi C. Endelea pia kufuatilia YouTube Channel yetu ya Dar24 Media mengi.

Masharti magumu yaliponza Kanisa, sasa kuburuzwa Mahakamani
Ulimwengu asepa Ulaya arudi Afrika kisoka