Kwa kawaida watu wengi wanapoenda kwenye usaili wa kazi hufikiria zaidi katika kujitetea kwa uwezo mzuri walionao katika kuifanya kazi iliyotangazwa huku wakisahau kuhusu upande wa pili wa swali hilo.

Kumbuka kuwa muajiri anaamini kuwa wewe ni binadamu wa kawaida na sio ‘robot’. Hivyo, mbali na kufahamu uwezo wako wa kufanya kazi angependa kufahamu upande wa pili wa maisha yako ya kawaida. Kwa kuwa hakufahamu, anaweza kukupa nafasi ya kujielezea mwenyewe mapungufu au udhaifu wako kama binadamu.

Uzoefu unaonesha kuwa karibia asilimia 90 ya waajiri/waasili huuliza swali hili katika usaili wa kazi. Nitakueleza sababu mwishoni mwa makala hii.

Unapaswa kuwa mkweli kiasi, eleza mapungufu hayo katika mtazamo chanya zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi. Kumbuka, kila unachoongea kwenye usaili lazima kiwe na lengo la kujiuza zaidi kwa mwajiri na sio vinginevyo.

Kwanza kabisa unapaswa kuzingatia aina ya kazi ili majibu yako yawe na mantiki wakati wote.

Kwa mfano, kama unatafuta kazi ya kuwa ‘meneja wa maudhui ya mitandao ya kampuni fulani’ (online content manager), unaweza kuutaja udhaifu wako wa kwanza kuwa ni uteja wa kukaa mtandaoni (online addict). Unaweza kueleza kuwa unafahamu uteja wa aina yoyote hautakiwi kabisa katika kazi hivyo huu ni udhaifu. Lakini uteja huu unaweza kuonekana kama faida kwa muajiri wa/kwa aina fulani.

Lakini, utakuwa umejiondolea sifa zote kama utatumia jibu hilo hilo katika usaili wa kumtafuta mtu anaetakiwa kuwafundisha watoto kuogelea.

Unaweza kufirikia nini kitatokea kama utakuwa unaperuzi mitandao muda wote wakati watoto wanaogelea.

Hata hivyo, yapo baadhi ya majibu ambayo unaweza kuyatoa kwa swali hilo katika usaili wa kazi yoyote. Nitatoa mifano ya majibu ya udhaifu wako katika mtazamo ulio chanya.

Cha muhimu, usijielezee sana wakati unataja udhaifu huu, na usionekane kama unajitetea sana badala ya kujibu ulichoulizwa.

Kwa mfano; siamini kabisa katika kushindwa. Naamini kushindwa ni uzembe na kukata tamaa. Lakini katika uhalisia, binadamu ana kikomo cha utendaji kwa hiyo nina udhaifu wa kushindana na uhalisia huo pale ninapotaka kutekeleza majukumu yangu. Kwa hiyo huwa nafsi yangu inashindana na uhalisia kuwa ‘kuna kushinda na kushindwa’.

Pili, sina Kiasi katika kazi. Kuna wakati nafanya kazi zaidi ya muda unaoshauriwa hata na wataalam wa masuala ya afya.

Tatu, ni msumbufu, huwa nageuka kuwa msumbufu pale ambapo ninapotaka kufahamu kitu fulani ambacho naamini kitanisaidia kukamilisha vizuri majukumu yangu. Ninapofahamu kuwa mtu fulani ndiye anayeweza kuwa msaada wa kunielewesha vizuri, humfuata kadri niwezavyo ili nipate maarifa ya kutosha kutoka kwake. Kwa wengine hii hugeuka kuwa usumbufu kutokana na kuwa na ratiba zao.

Ni mkamilifu kupitiliza, napenda kuona kazi yangu inafanyika kwa ukamilifu uliotukuka, hii hupelekea mara nyingi kutumia muda mwingi sana kuhakikisha nakamilisha jukumu langu kwa ubora uliotukuka. Hii hugeuka kuwa changamoto wakati mwingine kwa kazi ambazo zina ‘deadline’ ya kushitukiza.

interview

Kwa mifano hiyo naamini umeelewa vizuri njia sahihi ya kujibu swali hili ambalo huulizwa mara kwa mara na wasaili. Ingawa wapo wakosoaji wanaodai kuwa hii ni njia mtambuka ya kujibu swali hilo, bado majibu yanabaki kuwa muhimu kwa swali hilo.

Ni muhimu kutoa ufafanuzi wa jinsi gani utajiboresha ili kuweka sawa hicho ulichokitaja kama udhaifu katika kila unachokitaja. Elezea pia jinsi gani umeanza kuyafanyia kazi mapungufu hayo kwa kujifunza kila wakati.

Mambo ya kuzingatia wakati unachagua udhaifu wa kutaja

Usichague udhaifu wa kutaja kwa sababu tu ni mzuri kutamkika na kueleza jinsi utakavyoutatua, inabidi ufikirie zaidi. Usichague udhaifu ambao unaendana na vigezo vilivyowekwa na muajiri (required skills/ desired qualities).

Zingatia sana udhaifu unaoutoa, hakikisha unataja udhaifu ambao ni rahisi kuurekebisha kwa hali ya kawaida.

Kwa mfano, ni vyema ukasema kuwa, “Hujisikia uoga ninapokuwa naongea mbele ya umati mkubwa.” Huo mfano ni bora zaidi ya kusema, “Hujisikia aibu na kupata shida napoongea kwenye kikao.” Na usitaje kabisa udhaifu kama ‘kukosa umakini’.

Ni rahisi kuelezea jinsi ambavyo utauondoa uoga huo kuliko jinsi ambavyo utaiondoa aibu ya kuongea hata kwenye kundi dogo la watu kwenye kikao.

Kama unakumbuka mwanzo wa makala hii nilikuahidi kuwa nitakwambia sababu za kuulizwa swali hili. Unadhani kwa nini waajili au wasaili huendelea kuuliza swali hili wakati wanajua kabisa huenda majibu unayotoa sio ‘ukweli mtupu’?

Ukweli ni kwamba waajiri wataendelea kuuliza swali hili hata kama wanajua hutawaeleza ukweli mtupu kwa kuwa wanafahamu majibu yako yatawaeleza kitu cha ziada kuhusu wewe. Muajiri anaweza kusoma katikati ya mistari ya maelezo yako hayo.

Nini kitatokea endapo utashindwa kueleza udhaifu wako?

  • Muajiri anaweza kudhani unaudhaifu wa kutisha kiasi cha kushindwa kuutaja hadharani.
  • Muajiri anaweza kuhisi kuwa unadhani wewe ni mkamilifu kwa kuwa hauitambui nafsi yako.
  • Anaweza kufikiri pia kuwa unadhani wewe ni mkamilifu kwa sababu uelewa wako ni mdogo.

Kwa mifano hiyo michache, naamini unaweza kupata picha nzuri ya kujibu swali hili na kuonekana kuwa wewe ndiye chaguo bora zaidi kwa nafasi ya kazi iliyotangazwa baada ya kujibu maswali mengine vizuri.

 

Marotta Ampiga Kijembe Andrea Pirlo
Kocha Wa England Afichua Siri Za Arsenal