Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu amezitaka Halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kutekeleza miradi itakayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja badala ya kulipana posho za safari na vikao.

Waziri ummy ameyasema hayo Novemba 20, 2019 wakati alipotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya cha Hombolo kilichopo mkoani Dodoma na kusema Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo wanaunga mkono juhudi za kuboresha sekta ya afya hasa ile ya msingi.

Amesema Halmashauri hizo zinatakiwa kupambana kuhakikisha zinaleta mapinduzi katika mambo ya kimaendeleo hasa yale yanayoigusa jamii kwani itasaidia kuondoa kero mbalimbali zinazowakabili na kuongeza ufanisi wa utendaji kwenye masuala ya afya.

“Tumefika hapa leo tukiwa na lengo la kutembelea kituo hiki kuangalia huduma ambazo zinatolewa lakini nasisitiza Halmashauri zote badala ya kulipana posho za safari na mambo mengine sasa zijielekeze kufanya maendeleo yanayogusa wananchi moja kwa moja kwa kutumia mapato yake ya ndani,” amesisitiza Waziri Ummy.

Awali Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Dodoma Godwin Kunambi alimueleza Waziri Ummy kuwa walipokea shilingi milioni 500 zilizokamilisha majengo yote ikiwemo wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji, maabara, chumba za kuhifadhia maiti, na nyumba ya mganga mkuu.

“Na kwa kutumia mapato ya ndani tulitenga shilingi milioni 193 ambapo kwa kituo cha afya cha Hombolo tukapeleka zaidi ya shilingi milioni 60 zilizojenga wodi ya watoto na sasa kituo hiki kimekamilika kwani kuna wodi ya watoto na akina mama,” amefafanua Kunambi.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya cha Hombolo Dkt. Wende Mwakilusi amesema mpaka sasa mejengo yote ya hospitali hiyo yamekamilika kwa asilimia 100 na yameanza kutumika tangu mei 2, 2019 na kwamba mpaka sasa upande wa maabara umehudumia wateja 8,550.

Kuhusu huduma ya damu salama Dkt. Mwakilusi amesema hapo awali haikuwa ikipatikana katika kituo hicho cha afya lakini hivi sasa wanaendelea kuwahuduma wananchi wenye uhitaji wanaofika eneo hilo kwakua inapatikana kwa uhakika.

“Na mpaka sasa jumla ya wakina mama wajawazito wapatao 463 waliofika kituo hiki cha afya kwa huduma za masuala ya uzazi wamehudumiwa na kujifungua katika majengo haya ambapo 405 kati ya hao wamejifungua kwa njia ya kawaida na 58 wamejifungua kwa njia ya upasuaji,” amebainisha Dkt. Mwakilusi.

Wakiongea mbele ya Waziri Ummy baadhi ya Wagonjwa ambao wamekuwa wakipata huduma katika kituo hicho cha afya cha Hombolo wamesema kwa sasa hali ya upatikanaji huduma za afya inaridhisha ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.

Live: Kutunukiwa shahada ya udaktari wa falsafa kwa Rais Magufuli, Mahafali ya 10 UDOM
Misri, Ivory Coast kuiwakilisha Afrika Olimpiki 2020

Comments

comments