Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Kaimu Afisa Elimu (Msingi) wa wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, Bukuru Malembo awe amepeleka walimu wawili katika shule ya msingi iliyoko kwenye kitongoji cha Rwenzige kwa kuwa haina mwalimu hata mmoja.

Shule hiyo yenye madarasa mawili na ofisi moja ya mwalimu ina jumla wanafunzi 216 wa darasa la awali hadi la nne, ilijengwa na wananchi ambapo wanafunzi wake wanafundishwa na mwananchi mmoja aliyeamua kujitolea ili kuwapunguzia watoto kutembea umbali wa kilomita 16 kwenda kusoma katika shule ya kijiji cha Kiteme.

Ametoa agizo hilo baada ya wanafunzi wa shule hiyo kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya bango wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kiwanja cha kituo cha afya Kimeya, baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.

“Haiwezekani watoto wadogo wenye umri wa kuanzia miaka mitano wakatembea umbali wa kilomita 16 kwenda shule wakati katika kitongoji chao kuna shule yenye madarasa mawili na chumba kimoja cha ofisi ya mwalimu na Afisa Elimu hadi sasa hajapeleka walimu na kumuachia mwalimu Benson (kijana ambaye si mwalimu ila anajitolea kufundisha) akifundisha wanafunzi hao peke yake.”amesema Majaliwa

Amemuagiza Afisa Elimu huyo ahakikishe ifikapo Jumatano (Oktoba 10, 2018) saa nne asubuhi awe ameshawapeleka walimu hao katika shule hiyo ya msingi ili waweze kuwafundisha wanafunzi hao na kisha Mkuu wa wilaya hiyo, Mhandisi Richard Ruyango awasilishe taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo ofisini kwake.

Kwa upande wake, Benson Bukerebe (29) maarufu mwalimu Benson amesema kuwa yeye kitaaluma si mwalimu bali ni mhitimu wa kidato cha nne, aliamua kuanzisha darasa kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi hao kwani alikuwa akiwahurumia kwa sababu baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kutembea umbali wa kilomita 16 hadi iliko shule ya msingi ya Kiteme.

Amesema kuwa kwa muda wote huo ameweza kumudu kuwafundisha wanafunzi hao kwa kutumia vitabu vya kuazima kutoka shule mbalimbali za msingi, lengo ni kuhakikisha watoto wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji chao wanapata fursa ya elimu ambayo ni haki yao ya msingi.

Aidha, katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa Serikali imeweka sheria kali ili kuwalinda watoto wa kike na wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii kwa kuachwa waendelee na masomo yao bila ya usumbufu wa aina yoyote na atakayebainika kukatisha masomo yao atachukulia hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, ameongeza kuwa wazazi au walezi watakaowaozesha watoto kike ambao bado ni wanafunzi na kwa upande wa wazazi watakaomsindikiza mtoto wao wa kiume kwenda kuoa mwanafunzi wote watachukuliwa hatua za kisheria

Wanaowania Ballon d’Or 2018 wafahamika
Video: Watoto 400 wapotea ndani ya miaka 3, Wabunge 15 Ukawa wanaotajwa kuhamia CCM