Serikali ya Uganda inafikiria kuitambua Jamii ya Wahindi kama kabila ndani ya nchi hiyo, kutokana na historia ya kukaa miaka mingi ndani ya nchi hiyo na kuwekeza.

Akihutubia wiki hii ndani ya Ikulu ya nchi hiyo jijini Entebbe, katika kusherehekea Tamasha la Hindu of Lights au Diwali, Rais Yoweri Museveni amesema kuwa wanatafakari ombi la Umoja wa Jamii ya Kihindi kuhusu kuwatambua kama kabila.

Rais Museveni ambaye aliwaalika raia wenye asili ya India ndani ya Ikulu ilyoko Entebbe na kushiriki nao chakula, amesema kuwa suala hilo linaweza kujadiliwa na kuwekwa kwenye Katiba ya Uganda.

“Kwa upande wa suala la kuwatambua Wahindi kama kabila, Serikali inalifanyia kazi. Tunaweza kutumia mfano wa wa Nubi. Hawa walikuwa wanajeshi kutoka Misri, Uturuki na Sudan Kusini. Walikuja hapa na hawakurejea makwao. Wanafahamika kama kabila katika Katiba yetu,” amesema Rais Museveni, na kuandika kauli hiyo Twitter.

Aidha, Rais Museveni amewahakikishia kuwa mazingira ya kufanya biashara nchini humo yataendelea kuboreshwa na kwamba anatambua mchango wao katika biashara kwenye uchumi wa nchi hiyo. Alisema kuwa asilimia 80 ya makampuni makubwa nchini humo yanamilikiwa na Wahindi.

Mwaka jana, Umoja wa Wahindi nchini humo (Indian Association of Uganda), ulisema kuwa umeiandikia Serikali ombi maalum la kutaka watambulike kama sehemu ya makabila, kwani wengi wao wamekaa miaka mingi nchini humo.

Video: Mchungaji Moses Emena aiomba serikali kuwawezesha watoto wa kike
Video: Katibu Tawala wilaya ya Kinondoni awafunda wahitimu wa ufundi Cherehani