Baraza la Wadhamini la Klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake, George Mkuchika limependekeza klabu hiyo isifanye uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizowazi kwa sasa badala yake wafanye uchaguzi mkuu ili kupata viongozi wapya.

Ameyasema hayo mara baada ya kikao cha kamati ya utendaji na Baraza la wadhamini ambapo Mkuchika amesema kuwa wameazimia kuwaomba wanachama kufanya uchaguzi wake mkuu mwaka huu 2019 badala ya mwaka 2020.

Aidha, Mkuchika ameitaja sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kupisha uchaguzi mkuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2020.

”Maamuzi haya tunayapeleka kwa wanachama wote na wajumbe wa mkutano mkuu kwani sio busara kujaza mapengo mwaka huu kisha tena mwakani tufanye mkutano mkuu wa uchaguzi, tunaita mkutano wa wanachama wote ili wakikubali hili lifanyike kwa ridhaa yao isijekuonekana sisi tunawaburuza,” amesema Mkuchika.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa jambo hilo la kuwashirikisha wajumbe wa mkutano mkuu ili wapitishe pendekezo hilo linatakiwa kufanya haraka ikiwezekana ndani ya wiki tatu au nne.

Video: DC Kisare aupongeza mradi wa TACIP, awataka wasanii kuchangamkia fursa hiyo
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 14, 2019