Watanzania wameaswa kutokukubali kutumiwa na wanansiasa na kupelekea uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

Wito huo kwa watanzania umetolewa na Rais wa Shirika La Elimu ya Amani Tanzania, Wilison George akiwa ziarani mkoani Kagera, iliyolenga kulitambulisha shirika hilo kwa viongozi na wananchi mkoani humo.

George amesema shirika hilo limesajiliwa na serikali kwa ajili ya kutoa elimu ya Amani nchini.

Amesema amani iliyopo Tanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla, hivyo watanzania wana jukumu kubwa la kuilinda na kumuona anayetaka kuivuruga kama adui namba moja.

Rais huyo aliyeambatana na viongozi wengine wa shirika hilo ngazi ya Taifa, mkoa na wilaya, pia walifika ofisi za mkuu wa wilaya Missenyi na kumwambia mkuu huyo lengo la wao kufika hapo.

“Mkuu wa wilaya dhumuni kubwa la shirika hili ni amani, sisi ni walinzi wa amani, tunalinda amani kwa kutoa elimu, tangu tumeanza kufanyakazi tumeanza na vyama vya siasa ambavyo mpaka sasa migogoro yao imekwisha, hauwezi kuwa mlinzi wa amani halafu ukawa sababu ya kuvunjika kwa amani.” Alisema Rais George.

Rais Wilison amesema kuwa wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa elimu ya amani nchi nzima ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kutambua umuhimu wa Amani pale inapotoweka. Amesema mpaka sasa wamesambaa kwenye mikoa aaidi ya 22 nchi nzima.

“Utofauti wetu na mashirika mengine ni kwamba sisi tunafanya kazi na vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini na hao ndio wenzetu tunaofanya nao kazi, kwahiyo tunapata ushirikiano mkubwa kutoka kwenye vyombo hivyo na lengo letu tunahitaji tuwafikie watanzania wote waelewe umuhimu wa Amani, tunatamani siku moja polisi akae kituoni siku nzima asipatikane mwalifu, tunataka kwenye magereza yetu watu wanapungua hadi kuisha kabisa kwa kutojishughulisha na uhalifu.”

Kwa upande wa mkuu wa wilaya Missenyi Kanal Denisi Mwila amewashukuru viongozi wa shirika hilo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhubiri amani, ambapo aliahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi hao wakati wowote watakapohitaji uwepo wake.

Kanali Denis amesema kuwa uwepo shirika hilo hapa nchini utawasaidia viongozi hao kupambana na uhalifu kwa kuwa wananchi watakuwa na uelewa mkubwa wa vitu vinavyosababisha kuwepo uvunjifu wa amani.

“Wilaya yetu hii ya Missenyi, ipo mpakani ikipakana na nchi jirani ya Uganda kwa maeneo mbalimbali, changamoto ambayo ilikuwa kubwa katika wilaya hii ni pamoja na wimbi la uhamiaji haramu, uingizwaji holela wa mifugo kutoka nje ya nchi.”

“Tumeweza kuthibiti hali hiyo kwa nguvu kubwa, kwa mantiki hiyo nalishukuru shirika hili kufika hapa kwetu nina imani litatusaidia kuwaelimisha wananchi wetu kuhusu suala zima la kuilinda amani mkizingatia sisi huku tupo mipakani hivyo suala la kutoa elimu ya amani ni suala muhimu sana.” Alisema Kanali Mwila.

Sambamba na ziara hiyo shirika hilo pia lilitoa msaada wa vifaa kinga vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona katika shule ya sekondari Bunazi iliyopo wilayani Missenyi.

Misaada iliyotoewa shuleni hapo ni sabuni za kuanawia mikono, vitakasa mikono pamoja vifaa vya kuwekea maji.

Jose Mourinho ampigania Eric Dier
Serikali yataja mbinu zilizoingiza Tanzania uchumi wa kati "maamuzi magumu"

Comments

comments