Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi Tanzania (Veta) imetumia maendeleo ya teknolojia kubuni kifaa ambacho kitawalazimisha bodaboda na abiria wao kuvaa kofia ngumu (helmet).

Ubunifu huo umewekwa wazi kwenye maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, ambapo chuo hicho kimeeleza kuwa endapo kifaa hicho kilichobuniwa kitafungwa kwenye pikipiki, pikipiki hiyo haitawaka kama dereva na abiria wake hawatavaa helmet.

Mwanafunzi wa chuo hicho, Rentius Pesha aliyekuwa kwenye banda la chuo hicho, alisema kuwa ubunifu huo umeweka kifaa maalum kwenye kofia ngumu ambacho ndicho kinachobeba mfumo mzima wa utendaji wa pikipiki husika.

Alisisitiza kuwa mfumo huo hautaruhusu pikipiki kuwaka hata kama dereva na abiria watakuwa wameishikilia kofia ngumu au kuambatana nayo kwenye safari yao bali tu watakapoivaa kichwani.

“Dereva wa pikipiki pamoja na abiria wake wakivua kofia na wakiiweka sehemu nyingine hata kama ni katika hiyo pikipiki, haiwezi kuwaka,” Pesha anakaririwa.

Kwa upande wake mwalimu Anneth Mganga alisema kuwa anatamani Serikali iukubali na kuutumia mfumo huo, ili kuokoa maisha ya vijana wengi na abiria wanaotumia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.

“Hatua hii ikichukuliwa pia itasaidia kuwatia moyo wanaovumbua vitu mbalimbali kutoka kwenye vyuo vya ndani badala ya kusubiri wavumbuzi kutoka nje ndio wapewe sifa,” alisema mwalimu Mganga.

Hatua hii ya ubunifu ni jitihada za kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo la majeraha makubwa kwa bodaboda. Hivi karibuni, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ilieleza kuwa kwa wastani wamekuwa wakipokea majeruhi 20 wa bodaboda jijini Dar es Salaam.

Uvumbuzi huo wa kiteknolojia wa Veta ni muendelezo wa matokeo mazuri ya wanafunzi nchini kwani katika maonesho hayo pia wanafunzi kutoka chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) walionesha ugunduzi wa taa za kuongoza magari barabarani, ambazo zinaweza kuongoza magari kwa kuzingatia na kuruhusu kwa wingi sehemu ambayo kuna msongamano mkubwa zaidi wa magari.

Diamond: Hii ndio starehe yangu kubwa
Necta yatangaza matokeo kidato cha sita, yatazame hapa

Comments

comments