Tanzania tumetembelewa na ugeni wa aina yake kutoka Hispania, Klabu ya Sevilla ambayo kesho, Mei 23, 2019 itatinga dimbani na Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC hatua inayolisogeza Jicho la Dunia ya soka nchini Tanzania.

Mpambano huo ni sehemu ya kampeni ya ‘LaLiga World Challenge’ yenye lengo la kusambaza soka la Hispania duniani kutokana na kuongezeka kwa mashabiki wa ligi hiyo.

Sevilla imetua nchini na nyota wake 18 ambao ni tishio kwenye La liga. Baadhi yao ni Tomas Vaclík, Juan Soriano, Sergi Gómez, Kjaer, Gnagnon, Jesus Navas, Aleix Vidal, Escudero, Arana, Amadou, Roque Mesa, Banega, Franco Vazquez, Nolito, Promes, Bryan, Ben Yedder na Munir.

Timu hiyo yenye rekodi ya kunyakua taji la EUROPA mara tano ni klabu ya kwanza ya Hispania kukanyaga ardhi ya Tanzania na kucheza mechi ya kirafiki; na ni ya pili kutoka barani Ulaya baada ya Everton kushuka pia mnamo 2017 ilipochuana na timu bingwa Gor Mahia kutoka Kenya katika mashindano ya Sport Pesa.

Mtanange huo utatengeneza historia ya aina yake hasa endapo Simba itafanikiwa kuichapa klabu hiyo. Mabavu ya Simba dhidi ya Sevilla yanaweza kutafsriwa kutokana na matokeo mazuri ya hivi karibuni.

Mei 21, Simba waliichakaza Singida United kwenye dimba la Namfua, matokeo yaliyoifanya ijihikakikishie Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kadhalika, wekundu hao wa Msimbazi wana mtaji wa mafanikio ya kutinga katika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Afrika baada ya miaka 25.

Moja ya chachu ya ushindi kwa Simba wakiwa nyumbani ni nguvu kubwa ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiujaza Uwanja wa Taifa unaoingiza mashabiki Zaidi ya 60,000.

Je, Simba wataunguruma mbele ya wababe hao wa Sevilla na kuendeleza historia ya kutofungwa na timu za nje ya nchi kwenye dimba la nyumbani? Mpira ni dakika 90, lolote linaweza kutokea. Endelea kufuatilia Dar24 uwe wa kwanza kupata undani wa mechi hiyo. Usikose pia kutembelea YouTube channel yetu ‘Dar24 Media’.

Urais Indonesia: Sita wauawa, mamia wamejeruhiwa wakipinga matokeo
Video: Membe atesa kambi ya JPM, Magufuli awashukia vigogo mashirika 250

Comments

comments