Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imetajwa kuongeza tija katika utendaji wake kutokana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika huduma zake kwa wadau.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Prof. Lazaro Busagali ambapo amesema kuwa Tume hiyo imeimarisha utoaji wa huduma zake kwa wadau kuanzia katika utoaji wa vibali na huduma zote ikiwemo za maabara.
 
“ Tunaipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuiwezesha Tume kuwa na Ofisi za Kanda 21 na asilimia 90 ya vibali vinatolewa ndani ya siku moja kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu yetu ya kutolea huduma,“amesema Prof. Busagali
 
Amesema kuwa Teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri inaleta matokeo chanya katika jamii kwa kuwa ni muhimu katika kuchangia maendeleo kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo.
 
Aidha, amesema kuwa moja ya majukumu ya Tume ni kuhakikisha kuwa Taasisi zote zinazotumia mionzi katika kutoa huduma zake zikiwemo Hospitali zinazingatia matumizi bora ya mionzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hiyo.
Amefafanua kuwa, Tume imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi na wadau ili kuepuka matumizi ya mionzi yasiyozingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepusha madhara ya mionzi hiyo pale inapotumika vibaya.
“Serikali ya Awamu ya Tano imetuwezesha kuwa na maabara ya kisasa na pia wadau wetu ambao ni Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani kwa kutuwezesha kupata vifaa vya kisasa vya maabara yetu” Alisisitiza Prof. Busagali.
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ni Taasisi ya Serikali inayosimamia na kuratibu masuala yote yanayohusu mionzi hapa nchini ikiwa na maabara ya kisasa ambayo ni mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO)

Trump aeleza sababu ya kusitisha ghafla amri ya kuishambulia Iran
Video: Mbowe, wenzake wakwaa kisiki, Bajeti Z'bar yakuna wengi kutumia fedha za ndani