Tume ya Mipango imehitimisha mafunzo ya Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma yaliyowahusisha maofisa mipango wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri kutoka Mikoa ya Singida, Manyara na Dodoma yaliyofanyika tarehe 12-16 Septemba, 2016 katika ukumbi wa VETA mjini Dodoma.

Akifunga mafunzo hayo Kaimu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri aliwasihi washiriki kutumia ujuzi waliopata katika kuandaa, kutekeleza miradi ya Umma kwa njia za kisasa ili kuongeza ufanisi wa miradi na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Hata hivy alisema kuwa Tume ya Mipango imefanikiwa kutekeleza wajibu wake wa kuwajengea uwezo maafisa hao katika hatua zote muhimu zinazopaswa kuzingatiwa katika kufanya maandalizi, kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kufanya tathmini ya miradi ya maendeleo.

“Ni matumaini yangu kuwa hizi siku tano hazijapotea, mmepata elimu ya kutosha kutoka kwa wataalamu wetu katika masuala yote muhimu yanayohusu miradi ya Umma. Jukumu mlilonalo kwa sasa ni kuhakikisha mnatumia mbinu mlizofundishwa katika kutekeleza miradi ya serikali kwa usahihi ili tufikie malengo ya  mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano,” Alisema Bi Mwanri.

Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa wamepata elimu muhimu ambayo itarahisisha utendaji katika kusimamia miradi na kutoa ushauri wa kitaalamu katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

“vigezo kama mzunguko wa mradi ikiwa ni pamoja na andiko la awali, mchanganuo wa faida na hasara, vigezo vya kuchanganua mradi kama vile uwezo wa uzalishaji na thamani halisi ya uwekezaji vimetolewa ufafanuzi mzuri na vimeeleweka na tumevielewa” Alisema mshiriki mmoja James.

Tume ya mipango inaendelea na zoezi lake la kutoa mafunzo kwa walengwa wakuu ambao ni wataalam wa Sera na Mipango ambapo kuanzia Septemba 19 wataalamu wa mafunzo hayo watakua Mkoani mbeya kwa ajili ya zoezi hilo

Rais Mstaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi Aongoza Matembezi ya Hisani Kuchangia Wahanga wa Tetemeko la ardhi
Video: Prof. Benno Ndulu akitoa taarifa kamili ya hali ya uchumi Tanzania