Hatimaye Rais wa Marekani, Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un wamesaini mkataba wa awali wa tamko la pamoja nchini Singapore.

Viongozi hao ambao wameandika historia ya kuwa viongozi wa kwanza walioko madarakani wa nchi hizo zilizokuwa na mgogoro mkubwa wa mpango wa silaha za nyuklia, walikutana na kushikana mkono saa chache zilizopita.

Wawili hao walitoa kauli za kutia matumaini kuhusu kufanikiwa kwa mkutano wao. Trump alisema kuwa mkutano huo anaamini utazaa matunda mazuri huku Kim akieleza kuwa wamekubaliana kuhakikisha wanafanikisha nia njema.

Hatua ya kuonesha kwenye picha ya nyaraka iliyosainiwa kama tamko la pamoja imepata ukosoaji kutoka kwa wachambuzi mbalimbali ambao wamedai inaacha maswali mengi bila majibu.

“Ni vigumu sana kuona kila kitu kimewekwa kwenye ukurasa mmoja. Hakuna walipotaja kuhusu suala la vikwazo kwa Korea Kaskazini au undani wa mabadiliko ambayo wengi wanayatarajia,” alisema Malcom Cook, mchambuzi kutoka taasisi ya Lowy ya Australia.

Hata hivyo, picha ya tamko hilo inayoonekana imeelezwa kuwa Korea Kaskazini imekubali kufanyia kazi mpango wa kuondoa silaha za kinyuklia katika Rasi ya Korea na pia Rais Trump ameahidi kuihakikishia Korea Kaskazini usalama.

Maudhui ya tamko hilo bado hayajaachiwa rasmi kwa umma.

Video: Young Dee aahidi makubwa ''Hatutaki kufunikwa''
Jean-Michael Seri kucheza England msimu ujao?