Rais wa Marekani, Donald Trumpa amewashangaza washirika wake kwenye vita vinavyoendelea nchini Syria, baada ya kuamuru majeshi ya Marekani kurudi nyumbani haraka.

Trump ametekeleza azma yake hiyo jana akieleza kuwa kazi waliyofanya nchini Syria imetosha na kwamba wamefanikiwa kupata ushindi wa kihistoria dhidi ya kundi la kigaidi la Islamic State(IS).

Katika hatua nyingine, Rais Trump ameeleza kuwa amekuwa akipata shida kuwapigia simu na kuwaandikia barua wake, waume na wazazi wa wanajeshi ambao wamepoteza maisha katika mapambano nchini Syria.

“Tumewashinda ISIS, tumewapiga vibaya na tumerejesha ardhi. Sasa ni muda wa vikosi vyetu kurejea nyumbani. Nimekuwa napata majonzi ninapoandika barua au kuwapigia simu wazazi au wake au waume wa wanajeshi ambao wameuawa wakipigania nchi yetu,” Rais Trump ameeleza.

Hata hivyo, washirika wa Marekani katika vita hiyo wamekosoa vikali uamuzi wake kwa madai kuwa kitendo hicho kitasaidia kuwapa nafasi IS kujipanga upya kwani bado kuna masalia mengi ya kundi hilo kwenye baadhi ya maeneo.

Aidha, Seneta ambaye anatoka kwenye chama cha Republican, Lindsey Graham ameeleza kuwa uamuzi huo wa kujitoa ni kosa kubwa akieleza kuwa mbali ya kuipa nafasi IS, ni mwanya kwa mahasimu wao Urusi na Iran kuweka mizizi zaidi kwenye maeneo mengi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje wa Seneti, Bob Corker amewaambia waandishi wa habari kuwa ameshtushwa na uamuzi wa Rais Trump na kwamba hata alipojaribu kwenda Ikulu ili azungumze naye aliambiwa kikao chake na mkuu huyo wa nchi kimeahirishwa.

“Ni vigumu sana kupata picha kuwa rais yeyote anaweza kuamka asubuhi na kufanya uamuzi kama huo bila kufanya mawasiliano ya kutosha na kutokuwa na maandalizi ya kutosha,” amesema Corker.

Uingereza ambao ni washirika wakuu wa Marekani nao wameonesha kusita kueleza kuwa wamelitokomeza kundi la IS na kwamba wanapaswa kurejea nyumbani.

Urusi na Iran wana majeshi yao nchini Syria wambapo wanaunga mkono Serikali ya Bashar al-Assad ambayo inapingwa vikali na Marekani pamoja na washirika wao. Urusi na iran wanaendesha vita ya kumsaidia Assad dhidi ya makundi ya waasi pamoja na makundi ya kigaidi lakini pia wanamsaidia kumkingia kifua dhidi ya Marekani na washirika wake.

50,000 wapinga Kampuni ya Marekani kutumia maneno ya Kiswahili
Grace Mugabe aingia matatani, sasa atakiwa kukamatwa

Comments

comments