Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa Iran imefanya kosa kubwa sana kuitungua ndege ya jeshi la Marekani ambayo haikuwa na Rubani.

Amesema kuwa inawezekana kuwa Iran ilifanya kosa hilo la kibinaadamu lakini inawezekana haikukusudia kuitungua ndege hiyo.

“Ni vigumu sana kwangu kuamini kwamba tukio hilo lilikuwa la makusudi, lakini inazewezekana kabisa ilikuwa ni kosa la kibinaadamu, Yawezekana alikuwa ni mtu mmoja mpuuzi ndio alitoa amri ya kutungua ndege hiyo,” amesema Trump.

Aidha, Iran imesema kuwa ndege hiyo ya kijasusi ilikuwa ndani ya anga lake, lakini jeshi la Marekani limekanusha na kusema ilikuwa ikipaa katika anga la kimataifa.

Tukio hilo linaendeleza sintofahamu baina ya mataifa hayo mawili hususani katika eneo la mpaka baina ya Ghuba ya Omani na Ghuba ya Uajemi.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif amesema nchi yake itapeleka malalamiko Umoja wa Mataifa (UN) kuwa Marekani inavamia eneo lake.

Naye balozi wa Iran wa UN, Majid Takht Ravanchi amesema kuwa ni dhahiri kuwa ndege hiyo ilikuwa inafanya operesheni ya kijasusi wakati ikitunguliwa, kitu ambacho amesema ni uvunjifu wa wazi wa sheria za kimataifa.

Katika barua aliyomuandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Ravanchi amesema kuwa, japo Iran haitaki kuingia vitani, lakini ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya maadui.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameonya kuwa vita baina ya mataifa hayo mawili italeta janga ambalo madhara yake yatakuwa makubwa zaidi.

Vikosi vya Iran vilitangaza kuitungua ndege hiyo ya Marekani katika eneo karibu na Kuhmobarak katika jimbo la kusini la Hormozgan.

Hata hivyo jeshi la Marekani limeshikilia msimamo kuwa ndege hiyo haikuwa kwenye anga la Iran, na kusema ilikuwa ipo katika anga ya kimataifa kilomita 34 kutoka katika eneo la karibu na Iran.

Kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la Reuters, tayari Marekani imeshaanza operesheni ya kutafuta mabaki ya ndege hiyo iliyoangukia kwenye maji ya bahari ya kimataifa.

Vigogo 11 waikimbia nchi, Mbunge ang'aka maiti kutozwa fedha hospitali
LIVE: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma