Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC),  Masanja Kungu Kadogosa ameruhusu treni ya kwanza ya mizigo kuashiria kurejea kwa huduma ya usafiri wa treni za abiria na mizigo kati ya Kilosa – Gulwe.

Tukio hilo limefanyika Kilosa mkoani Morogoro kufuatia kusitishwa kwa Huduma za usafiri wa treni za abiria na mizigo kwa takribani wiki mbili na nusu kutokana mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kuharibu miundombinu ya reli.

Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua zilizotajwa kunyesha kwa wingi katika Mikoa ya Iringa, Manyara, Singida na Dodoma na kupelekea kuongezeka kwa maji katika mto Mkondoa na kuisomba reli ikiwa ni pamoja na kuharibu tuta 120, ikiwemo kuharibika kwa makalavati, reli, stesheni, na madaraja.

Shirika limefanya jitihada za kuhakikisha huduma inarejea haraka iwezekanavyo kwa kutuma kikosi kazi cha mafundi na wahandisi wa kutosha katika eneo hilo ambapo wataalamu hao walikuwa wakifanya  kwa kushirikiana na wahandisi wa mkandarasi kampuni za CCECC inayoboresha reli ya kati pamoja na YAPI MARKEZI inayojenga reli ya kisasa, ambao wote kwa pamoja wameshirikiana kurejesha huduma ya usafiri kwa njia ya reli.

Hata hivyo mkurugenzi ameweka bayana kuwa njia iliyofunguliwa ni ya muda kutokana na uharibifu kuwa mkubwa na baada ya hapo Shirika litajikita kuimarisha na kutengeneza njia ya kudumu ambayo itakuwa ni suluhisho la mafuriko yanayotokea na kuharibu miundombinu ya reli katika maeneo ya Kilosa.

Kwa upande wake Mhandisi Felician Hechei, Meneja Mradi uboreshaji wa reli ya kati Kilosa – Gulwe ameeleza namna kazi ya uboreshaji reli ilivyofanyika kwa kuzingatia ubora na uimara wa eneo kutokana na miundombinu ya reli kuharibika kwa kiasi kikubwa.

Aidha, wahandisi walizingatia sehemu ambazo wanaweza kurudisha njia kwa wepesi ikiwemo kuangalia maeneo yenye uimara ambayo yaliwezekana kuweka tuta la reli upya, lakini pia maeneo yaliyoharibika kwa kina kirefu walihamisha.

Rais wa zamani wa Misri afariki dunia
RC Mtwara ataka kuboresha pombe ya gongo