Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) imesema endapo mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC wataomba wapelekewe kombe la ubingwa kabla ya msimu kumalizika, watawawekea utaratibu.

Simba SC mwishoni mwa juma hili watacheza dhidi ya Tanzania Prisons mjini Mbeya, na endapo watashinda watafikia lengo la kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2019/20.

Klabu hiyo ya Msimbazi ikitetea ubingwa huo keshokutwa Jumapili, itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kulibeba kombe hilo, katika misimu ya hivi karibuni wakianza msimu wa 2017-18.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania(TPLB), Steven Mguto amesema kwa utaratibu ambao wamejiwekea hawatawapelekea Simba kombe katika Uwanja wa Sokoine Mbeya Jumamosi hata kama watashinda.

Amesema utaratibu wao ambao wamejipangia kuwa wanataka kuwakabidhi mabingwa kombe pamoja na sherehe zote katika mechi yao ya mwisho lakini kama watataka vinginevyo wapeleke maombi rasmi.

“Kama kuna mechi ambayo wanataka wakabidhiwe ubingwa wao watatuletea maombi hayo lakini kwetu tulipanga kuwapa kombe pamoja na sherehe kiujumla katika mechi ya mwisho,” alisema Mguto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Coastal Union ya Tanga.

Hata hivyo uongozi wa Simba SC umesema utafanya kikao cha ndani, ambacho kitatoa maamuzi ya wapi watakapokabidhiwa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2019/20.

Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa amesema baada ya kikao hicho, Simba SC itatoa tamko rasmi, na kuwafahamisha mashabiki na wanachama wao, ambao wana shauku ya kujua ni wapi watajumuika na timu yao siku ya kukabidhiwa taji la ubingwa.

“Tutakutana viongozi na tutafanya kikao cha ndani ambacho ndio kitatoka na majibu kwamba tunaweza kusubiri hadi mechi ya mwisho ndio tukabidhiwe kombe pamoja na kufanya sherehe za ubingwa au tufanye maombi ya kuchukua katika mechi fulani.” Amesema Senzo.

Simba SC wamecheza michezo 32, na kufikisha alama 78 huku wakisaliwa na alama tatu tu kumaliza kazi bila kuangalia matokeo ya timu yoyote.

Dodoma FC waipongeza TPLB
Eymael afichua kinachoisumbua Young Africans