Kocha mpya wa kikosi cha Cameroon (Indomitable Lions) Toni Conceicao, amejinasibu kuwa tayari kwa mapambano ya soka la Afrika, ili kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa bara hilo, kupitia fainali za AFCON 2021.

Conceicao alitangazwa kuwa kocha mkuu wa kikosi cha Cameroon mwishoni mwa juma lililpita, akichukua nafasi ilioachwa wazi na   Clarence Seedorf, alietimuliwa mwezi Julai, kufuatia kushindwa kufikia lengo la kuipa mafanikio ya kutwaa ubingwa wa AFCON 2019 Indomitable Lions.

Kocha huyo kutoka nchini Ureno, amesema jukumu lililo mbele yake ni kubwa, lakini anaamini kwa ushirikiano anaoutarajia kutoka kwa viongozi wa shirikisho la soka na wachezaji wake, atafanikiwa.

“Kila kazi ina changamoto zake, unachotakiwa kufanya ni kupambana bila kukata tamaa, huku ukitegemea ushirikiano kutoka kwa viongozi na wachezaji watakaounda kikosi kwa ajili ya mapambano,” alisema kocha huyo aliyewahi kukinoa kikosi cha klabu ya CFR Cluj.

“Nitahakikisha kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake, japo mwisho wa siku nitatazamwa mimi kama shujaa ama muhanga wa kushindwa, lakini nina uhakika kazi itafanyika na itaonekana,”

“Hii nafasi ni ya kipekee kwangu, ninahitaji kuitendea haki kadri nitakavyoweza, najua wananchi wa Cameroon wanafahamu raha ya kuwa bingwa wa michuano mikubwa kama AFCON.”

Conceicao, atasaidiwa na gwiji wa Cameroon Francois Omam-Biyik, ambaye alikua sehemu ya kikosi kilichotwaa ubingwa wa AFCON mwaka 1988.

Naye mlinda mlango wa zamani wa klabu ya Deportivo La Coruna ya Hispania na Metz ya Ufaransa Jacques Songo’o, atakuwa sehemu ya benchi la ufundi la Cameroon.

Benchi jipya ya ufundi la Cameroon likiongozwa na Conceicao, litaanza kazi yake mwezi Novemba katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Afrika, dhidi ya Cape Verde.

Cameroon watakua wenyeji wa fainali zijazo za Afrika (AFCON 2021), na azma yao kubwa ni kubakisha ubingwa wa fainali hizo nyumbani kwao.

Ngorongoro Heroes yaipania Zanzibar
Rais Magufuli afanya uteuzi mwingine NBS