Shirikisho la soka nchini TFF limetangaza kifo cha aliyekuwa mtunza vifaa msaidizi wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Kessy Rajab kilichotokea jana Desemba 23.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, zinaeleza kuwa chanzo cha kifo hicho ni mshtuko alioupata katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika, kati ya Simba na Nkana Red Devils uliopigwa katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Rajab Kessy ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba alihudhuria katika mchezo huo wa jana, alipata mshtuko mara baada ya Simba kufungwa bao la kwanza, alikimbizwa hospitali ya Temeke ambako ndipo alipoteza maisha.

Hata hivyo mwisho wa mchuano huo mkali, timu ya Simba iliibuka na ushindi wa mabao matatu kwa moja na kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya klabu Bingwa Afrika.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania TFF Wallace Karia amepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa kifo cha aliyekuwa mtunza vifaa msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Kessy Rajab”.

Kwa niaba ya TFF, Rais Karia ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Kessy, ndugu, jamaa, marafiki na watumishi wenzake.

Kwa taarifa zilizotolewa msiba upo nyumbani kwake, Kurasini karibu na Uhamiaji wakati taratibu nyingine za mazishi zikiendelea.

 

Aliyemwagiwa tindikali na mpenzi wake awaburuza polisi Mahakamani
Kolasinac: Ozil amewanyamazisha, tuko nyuma yake