Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA) imekanusha tuhuma za Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Ndege ya Fastjet Tanzania, Lawrence Masha, ambaye alidai kuwa Mamlaka hiyo imewazuia kuingiza ndege mpya nchini Desemba 22 mwaka huu kama walivyokuwa wamewaahidi wateja wao.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamza Johari amesema kuwa Fastjet Tanzania hawajazuiwa kuingiza ndege bali maombi yao bado yanashughulikiwa.

Alieleza kuwa tangu walipotoa tangazo la nia ya kuifuta Fastjet Novemba 17 mwaka huu, Uongozi wa kampuni hiyo ya ndege uliwasilisha andiko lao la maombi ya kuendelea na biashara hiyo Desemba 24. Hivyo, alisema bado Mamlaka hiyo inayafanyia kazi.

Alieleza kuwa Fastjet wameshalipa baadhi ya madeni yao kati ya Sh6 bilioni walizokuwa wanadaiwa na watu mbalimbali, lakini hawajakamilisha malipo ya madeni yote.

Johari alisisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia masharti ya uendeshaji wa usafiri wa anga kwani bila kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha ya watu; na kwamba kama shirika hilo halitakamilisha masharti leseni yao itafutwa.

“Miongoni mwa mambo ya msingi ni uwezo wa kifedha katika shirika, usafiri wa anga hakuna ujanja kama hatakidhi masharti leseni yake itafutwa. Tukisema tuhurumiane ni hatari tutaua watu, usafari wa anga usiposimamiwa vizuri ni hatari kwa usalama wa watu,” alisema Hamza.

Jana, Masha aliwaambia waandishi wa habari kuwa Serikali imezuia kuingizwa kwa ndege mpya za Fastjet, huku akiweka matumaini kuwa baada ya msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka huenda wakafanikiwa.

Nguvu ya imani na subira 2019
Mipango ya mafanikio hufa katika hatua hii