Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji ambao bidhaa zao zimekidhi matakwa ya viwango na kukabidhiwa leseni za kutumia alama ya ubora,  kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kupanua masoko yao ikiwa pamoja na kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

 Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Profesa Makenya Maboko, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Viwango Afrika (ARSO) yaliyofanyika makao makuu ya shirika, hilo Ubungo jijini Dar es Salaam.

 Amesema kuwa alama ya ubora ni muhimu sana katika biashara kwani inampa mzalishaji uhakika kuhusiana na ubora na usalama wa bidhaa yake, hivyo kumjengea imani kwa walaji.

“Lakini pia alama ya ubora humsaidia mzalishaji kupanua masoko ya bidhaa zake nje ya nchi, ni wazi basi hatua hii ni ya kujivunia sana kama mzalishaji, kama Taifa kupanuka kwa masoko  ya kikanda na kimataifa kutasaidia kuongeza fedha za kigeni, hivyo kusaidia kukuza uchumi.”amesema Prof. Maboko

Kuhusu jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli, katika kupambana na rushwa nchini, Profesa Maboko, amesema kuwa wao kama wadau wa viwango ni fursa muhimu ya kuhakikisha wanatoa mchango wao kwa kueneza uelewa na weledi unaotumika katika kuandaa viwango na pia kuwahamasisha wazalishaji na watoa huduma kuhusu umuhimu wa kuzingatia matakwa ya viwango katika shughuli zao.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya amesema kuwa wao kama taasisi Siku ya Maadhimisho ya Viwango Afrika ni muhimu, kwani wanapata fursa ya kuwakumbusha wazalishaji, watoa huduma na wananchi wote kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua katika suala la vita dhidi ya rushwa, hivyo na wao katika tasnia ya viwango, wanayo fursa ya kuonesha njia katika kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa, hivyo kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika ipasavyo katika kuondoa wananchi katika umaskini na kuwaletea maendeleo.

Kauli ya Trump yazua utata kuhusu milima Golan
Kwasasa hatuhitaji kuungwa mkono na mbunge yeyote- CUF

Comments

comments