Mbunge wa Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete amesema kuwa imechukua miaka 16 kwa wananchi wa Chalinze kupata majisafi na salama na imani yake kubwa ipo kwa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA kufanikisha mradi huo.
 
Ameyasema hayo, mara baada ya kutembelea kiwanda cha mabomba cha Tanzania Steel Pipes kinachotengeneza mabomba ya kusafirishia maji kwenye mradi wa maji wa Mlandizi- Chalinze- Mboga.
 
Amesema kuwa amefurahishwa na maendeleo ya utengenezaji wa mabomba hayo ambapo takribani mabomba 321 yameanza kusafirishwa kwa ajili ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kuanza katikati ya mwezi April. mwaka huu.
 
“Sikuwahi kuona namna wananchi wanatumia maji pamoja na wanyama kama ng’ombe ila kukamilika kwa mradi huu kutawezesha watu kupata majisafi na salama,”amesema Ridhiwani
 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka DAWASA Mhandisi, Arone Joseph amesema kuwa mradi wa maji wa Mlandizi -Mboga unatarajiwa kusafirisha maji lita milioni 9.3 (mita za ujazo 9300) kwa siku kiasi kianchokisiwa kuweza kutosheleza mahitaji ya walengwa kwa sasa na ongezeko la matumizi kwa siku za usoni.
 
Aidha, amesema kuwa hadi sasa, kiasi cha mabomba ya umbali wa km 3.7 yameshazalishwa katika kiwanda cha TSP na yameanza kupelekwa kwenye maeneo ya mradi ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza katika Vijiji vya Mboga na Msoga.
 
Maeneo yatakayohudumiwa na mradi huo ni pamoja na Ruvu darajani, Vigwaza, Ranchi ya Taifa Ruvu (NARCO), Chahua -Lukenge, Visenzi, Buyuni na Mdaula -Unebazomozi, ambapo maeneo mengine ni pamoja na Chamakweza, Pingi, Pera, Chalinze, Chalinze Mzee, Msoga na Mboga, huku viwanda vitakavyofaidika ni pamoja na Twyford, kiwanda cha ngozi, kiwanda cha Matunda cha Sayona pamoja na watumiaji wengine wakubwa ikiwemo kampuni Yapi Merkezi wajenzi reli ya kisasa (SGR).

Hatari! Upasuaji chanzo kikuu vifo Wanawake
Ofisi ya makamu wa Rais yapongezwa kwa jitihada za kutunza mazingira