Kamanda wa polisi kanda maalum jijini Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu saba vilivyotokea kufutia mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es salaam kwa mfululizo na kusababisha mafuriko.

Kufuatia vifo hivyo, Mambosasa amesema kwamba mwili mmoja umekutwa ukielea kuelekea maeneo ya Jangwani jijini Dar es salaam.

Sambamba na hilo Kamanda Mambosasa amesema maeneo mengi jijini Dar es salaam yamejaa maji, na kuwataka watu kuwa makini wanapotumia barabara hasa sehemu zenye makorongo, na kuwaangalia zaidi watoto ambao wanapita mara kwa mara wakienda shule au wakiwa wanarudi kutoka shule.

“Watu wasijaribu maji, ukijaribu maji ujue utaondoka nayo, kwa hiyo watoto wetu wanapokwenda shuleni tuwasindikize, sehemu nyingi zenye makorongo kwa mfano kule Kinyerezi, kule Goba kule Makongo, zile shortcut zote maji yamejaa, watu wajiepushe kutumia njia hizo, watapoteza watoto wakiwa wanaenda au kutoka shule”, amesema Kamanda Mambosasa.

Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa taarifa za sehemu mbali mbali kuhusu hali ya mvua, ambayo inaendelea kuathiri sehemu kubwa ya nchi.

Mshairi atupwa jela miaka 3 kwa kuhamasisha umoja
Mwanasiasa mkongwe nchini Kenya afariki dunia