Tasnia ya Muziki nchini imepata pigo kwa kumpoteza Golden Mbunda maarufu kama Godzilla, aliyefariki usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam.

Ingawa bado haijatolewa taarifa rasmi ya chanzo cha kifo cha rapa huyo mahiri, watu wa karibu wa msanii huyo wameleeza kuwa chanzo cha kifo chake ni shinikizo la damu pamoja na tatizo la tumbo.

Mtu wa karibu wa Msanii huyo aliyejitambulisha kwa jina la Isabella ambaye alikuwa naye mara ya mwisho jana, saa chache kabla ya kufariki dunia, amesema msanii huyo alizidiwa ghafla akiwa nyumbani kwao maeneo ya Salasala jijini Dar es Salaam.

“Jana nilikuwa naye, nilivyoondoka usiku walimpeleka kwenye Dispensary, baadaye wakamhamishia Lugalo [Hospital], amefariki akiwa Lugalo,” Isabella amekaririwa.

Akizungumzia chanzo cha kifo chake, amedai kuwa Godzilla alikuwa akilalamika tumbo na kwamba presha ilipanda. Hata hivyo, tunasubiri taarifa rasmi za kidaktari na familia.

Godzilla alikuwa mwamba wa mitindo huru (freestyle) na aliyefanikiwa kufanya ngoma kubwa na wimbo wa ‘Stay’ ulikuwa moja kati ya nyimbo zake za mwisho kuachiwa rasmi.

Baadhi ya nyimbo zake kubwa ni ‘Jinsi nilivyo’, ‘First Class’, ‘Mama I made It’, ‘Milele’ feat Ali Kiba na ‘Nataka’.

Dar24 imeguswa na msiba huu mzito kwenye tasnia ya Muziki na tunatoa pole kwa familia, ndugu na kila mdau wa sanaa. Tunamuomba Mungu ampumzishe kwa amani King Zilla.

Solskjaer afunguka baada ya kupigwa na PSG nyumbani
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 13, 2019

Comments

comments