Na: Nelson Kessy

Tanzania na Kenya zimeahidi kuendeleza na kushirikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo baina ya nchi hizo yanakuwa kila wakati.

Akihutubia sherehe za maadhimisho ya 56 ya Jamhuri ya Kenya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Tanzania na Kenya ni ndugu na nchi hizo zitaendelea kushikiana katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya diplomasia ya uchumi yanakuwa kila wakati.

“Sisi Tanzania na Kenya ni ndugu wa damu, kwa hiyo basi tunawatakia sana kila la kheri katika kuiletea Kenya maendele, lakini mjue kuwa maendeleo ya Kenya ni maendeleo ya Tanzania pia; na maendeleo ya Uganda ni maendeleo pia ya Burundi, Rwanda, Sudani Kusini; na ni maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wake Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa umoja na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa Kenya na kusema kuwa umoja huo umekuwa ni chachu ya maendeleo kwa Tanzania na Kenya.

“Napenda kuwafahamisha kuwa umoja na mshikamano wetu umekuwa chachu ya maendeleo baina ya mataifa haya mawili…tukumbuke kuwa umoja ni nguvu na dhamira yetu ni kushirikiana na mataifa yote duniani. Na dhamira yetu ni kuishi kwa amani umoja na mshikamano ili kukuza uchumi wetu,” amesema Balozi Kazungu.

Aidha, Balozi Kazungu amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa ya kipekee kwa taifa la Kenya kutokana na mshikamano ambao imekuwa ikionesha kwa nchi ya Kenya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu akigonga glasi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ikiwa ni ishara ya upendo, umoja na mshikamano baina ya nchi hizo mbili mara baada ya kuzindua rasmi maadhimisho ya miaka 56 ya Jamhuri ya Kenya jijini Dar es Salaam

“Itakumbukwa kuwa, mwezi Aprili 2019 Kenya tulipokutana na Tanzania jijini Arusha tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara 25 kati ya 37, hii inadhihirisha ni kwa jinsi gani Kenya na Tanzania na ndugu ambao wanapenda kukuza na kuendeleza maendeleo ya biashara” ameongeza Balozi Kazungu.

Uchambuzi: Nani mshindi Real Madrid Vs Valencia Jumapili hii?
Ole Sendeka aagiza wadaiwa sugu wa NJOCOBA kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi