Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefuta maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Elimu yanayoelekeza Nembo na Wimbo wa Taifa kutumika kwenye dhifa za kitaifa pekee, ambayo pia yanaelekeza kuwa rangi ya njano katika Bendera ya taifa inatakiwa kuwa rangi ya dhahabu badala ya njano ya sasa.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema kuwa barua hiyo iliyotolewa na Wizara ya Elimu inaathiri uzalendo wa Watanzania na inaleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo kwenye bendera ya Taifa.

“Barua hiyo yenye kichwa cha habari, ‘MATUMIZI SAHIHI YA BENDERA, NEMBO NA WIMBO WA TAIFA’ imetoa maelekezo ambayo hata mimi mwenyewe tangu nasoma shule hadi leo nafahamu kuwa bendera ya taifa ina rangi ya njano na sio ya dhahabu, na rangi hiyo ya njano inawakilisha madini yote na sio dhahabu peke yake”, amesema Rais Magufuli kwenye taarifa hiyo ya Ikulu

Hayo yanajiri kukiwa na sintofahamu juu ya kusambaa kwa barua mitandaoni,  ambayo imeandikwa Novemba 23 mwaka huu ikiwa na kumbukumbu namba CHA-56/193/02/16, ambayo inasema wizara hiyo imepokea barua ya maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhusu matumizi sahihi ya bendera na Nembo ya Taifa, na Wimbo wa Taifa.

Video: Bunge la Ulaya laiwekea Tanzania mazimio15, Uchaguzi mkubwa benki zote nchini
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Desemba 15, 2018