Wananchi 203 wa kijiji cha Kandoto wilayani Same waliokuwa wakidai Fidia wamelipwa kiasi cha shilingi billion 1.99 na shirika la umeme Tanzania (TANESCO), jana februari 11, 2020.

Akizungumza wakati wa utoaji fidia hizo Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Mahawa Mkaka amesema eneo hilo lilikuwa ni mali za wananchi 301 waliopaswa kulipwa fidia ya Sh 3.5 bilioni lakini wameanza awamu ya kwanza na wananchi 203 ambao wamelipwa Sh1.99 bilioni.

Hayo yamejiri baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kutoa agizo kwa TANESCO mwezi Julai mwaka Jana akiwa kwenye ziara ya kikazi Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu kuwalipa fidia wananchi 203 wa kijiji cha Kandoto Wilayani humo baada ya mashamba yao kuchukuliwa na shirika hilo kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kutumia Jua.

Majaliwa alitoa maagizo hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliodai kuchukuliwa eneo lao la ekari 100 na kukubali kupisha ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Jua unaotarajiwa kuzalisha megawati 150 zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Wakizungumzia malipo hayo, Zenobia Msangi na Ayubu Abdalla mbali na kuishukuru Serikali kwa hatua iliyochukua na kuwezesha kulipwa fidia zao, wamesema fedha walizopewa watazitumia kuanzisha miradi ya maendeleo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi. “Tulianza kudai fidia mwaka 2016 tulifika mahali tukakata tamaa, tukidhani hatutalipwa lakini leo tumelipwa kila mtu haki yake aliyostahili, tunaishukuru sana Serikali, kwa hatua hii,” amesema Zenobia.

Mfanyabiashara apigwa faini mil.9 kwa kukosa mashine ya EFD
Mazishi ya Kobe Bryant na Gianna yafanyika kimya kimya

Comments

comments