Takwimu zinaonesha asilimia 39.4 ya Kata, Mitaaa na Vijiji nchini, imekuwa ikiongoza kwa rushwa  ikifuatiwa na secta ya  ardhi asilimia 13.5 na Elimu  kwa asilimia 12.3, takwimu ambazo zinatolewa ikiwa mwezi mmoja kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajia kufanyika nchini Novemba 24 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo oktoba mosi jijini hapa, na Mkuu wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Dodoma Sosthenes Kibwengo, na kuongeza kuwa tuhuma nyingine zilizobaki zinahusu sekta ya Afya, Uhamiaji, Tarura na Vyama vya siasa.

Amesema tuhuma za rushwa zilizo ripotiwa katika maeneo ya Mahakama ni asilimia 7.7, Polisi asilimia 5.2, Wizara kwa asilimia 5.8, Maji asilimia 4.5 na Sekta binafsi kwa asilimia 5.2, katika kipindi cha Julai hadi septemba mwaka huu.

“Tuhuma hizi ni kwa kipindi cha robo ya mwezi Julai hadi septemba mwaka huu ambapo tulipokea jumla tuhuma 155 na tayari tumekamilisha majalada 15 ya uchunguzi na kufungua mashauri 8 mahakamani,” amefafanua Kibwengo.

Amewataja wahusika wa tuhuma hizo kuwa ni watumishi wa sekta za Kilimo, Nida, Elimu, Watendaji wa Kata na Vijiji, Askari wa Jeshi la Akibs, Tanroads na watu binafsi.

Aidha katika kupambana na kuzuia rushwa, Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma amesema wamefuatilia miradi 39 ya maendeleo, yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 46 katika sekta ya ujenzi wa Elimu, Maji, Afya, Kilimo na miundombinu na kubaini uwepo wa viashiria vya rushwa.

“Kutokana na mazingira ya uwepo wa viashiria vya Rushwa, TAKUKURU imeingilia kati utekelezaji wa mkataba wa uundwaji wa kampuni kati ya Halmashauri moja na Taasisi binafsi, ambapo walipanga wanunue maeneo, wayapime kwa ajili ya kuuza viwanja, mkataba huu ungeweza kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya shilingi Milioni 700,” ameongeza Kibwengo.

Wakati huohuo, TAKUKURU mkoani Dodoma, inamshikilia aliyekuwa Afisa Afya na Mratibu wa mradi wa Belgian Fund for Food Security (BFFS) wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi  Emanuel Mziwanda (60), kwa kosa la kugushi, kumdanganya muajiri wake na kuisababishia Serikali hasara ya Shilingi Milioni 15.

Azam Fc sasa kugeukia ligi kuu bara
Yanga yatangaza kamati mpya ujenzi na miundombinu