Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha mwishoni mwa wiki hii katika maeneo mbalimbali ya nchi na imewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Meneja wa Utabiri Samuel Mbuya amesema mvua hiyo ni mwendelezo wa mvua ya masika inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kutonyesha mwezi uliopita kutokana na ujio wa kimbunga Keneth kilichobadili hali ya hewa.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari mapema huku wakiendea kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Mbuya amesema juzi kipimo cha kupimia mvua cha Pemba kilionyesha kiasi cha mvua milimita 105.3 na hadi kufikia jana iliongezeka na kufikia milimita 181, huku kituo cha kupimia mvua kilichopo uwanja wa ndege (JNIA) Dar es salaam, juzi kilipima milimita 64.4 na jana iliongezeka hadi  mililita 79.0.

Amesema kutokana na hali hiyo mvua itakayonyesha mwishoni mwa wiki hii itafikia vipimo hivyo au kuongezeka zaidi hasa katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga, Zanzibar na Pemba.

Aidha ameeleza kuwa katika mikoa ya nyanda za juu kusini na mikoa ya kanda ya ziwa itaendelea kupata mvua ya masika kama kawaida hivyo basi wakulima wanapaswa kufuatilia taarifa zaidi ya hali ya hewa.

UN yazindua njia mpya ya kuthibiti ugaidi
Serikali kuendelea kutoa elimu bora ya Kilimo