Kikosi cha Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC kimeanza maandalizi ya mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaochezwa mkoani Morogoro mwishoni mwa juma hili.

Simba SC wameanza maandalizi ya kuelekea mpambano huo, baada ya kurejea jijini Dar es salaam juzi Jumatatu, walikocheza mchezo wa mzunguuko wa kwanza dhidi ya Ihefu FC ambao walikubali kichapo cha mabao mawili kwa moja.

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kikosi chake kitaingia tofauti katika mchezo huo utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani humo.

Kocha Sven, amesema tayari ameshaanza kuyafanyia kazi mapungufu aliyoyaona katika mchezo wa kwanza dhidi ya Ihefu FC, ambayo yalionekana kuwapa ahuweni wapinzani wao kufika langoni mwa Simba mara kwa mara.

“Kwenye mchezo wetu tuliocheza Mbeya, kikubwa kilikuwa kupata alama tatu, tunashukuru tumezipata, lakini kama kocha nimeona yapo ambayo ni dosari kidogo ambazo nazifanyia kazi kabla ya mchezo wetu ujao,” amesema Sven.

Kocha huyo ameeleza mapungufu mengine aliyoyaona kwenye kikosi chake yalikuwa katika safu ya ulinzi na anaamini kuelekea mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar hayatajirudia.

“Kuna baadhi ya mapungufu kwenye safu yangu ya ulinzi, ninaamini yataondoka ndani ya muda mfupi na tutakuwa na mchezo mzuri siku ya Jumamosi,” amesema kocha huyo kutoka Ubelgiji.

Baraza atoa kongole Biashara United Mara
Urusi yaogopa vikwazo vya G7