Mabingwa wa soka Tanzania bara Wekundu Wa Msimbazi Simba (Simba SC), wapo katika mpango wa kutaka kumng’oa kocha wa Polisi Tanzania FC Suleiman Matola, ili wamkabidhi jukumu la kuwa kocha mkuu.

Uongozi wa Simba SC upo katika mpango huo, baada ya kuthibitisha kuachana na kocha Patrick Aussems jana Jumamosi (Novemba 30).

Matola anapewa kipaumbele cha kurithi mikoba ya kocha mkuu huko Msimbazi, kufuatia kuwa na uzoefu wa kutosha katika ligi ya Tanzania bara, pamoja na kuifahamu vyema klabu ya Simba, ambayo aliwahi kuitumikia kama mchezaji.

Hata hivyo makamu mwenyekiti wa Polisi Tanzania FC Robert Munis, alipoulizwa kuhusu mpango huo wa mabingwa mara 20 wa Tanzania bara, alisema hakuna shaka yoyote endapo watakubaliana na uongozi wa Simba.

“Matola bado ana mkataba na Polisi Tanzania, lakini kama Simba SC wanamuhitaji itawapasa wafuate taratibu za kulipa fidia za kuvunja mkataba wa kocha wetu,” alisema Munis alipohojiwa na gazeti la Mwanaspoti.

“Hatuna sababu yoyote ya kumzuia Matola, endapo kila hatua itafuatwa kikamilifu, soka ni mchezo unaotoa ajira kila kukicha, na kama bahati imeangukia kwa Matola na ina maslahi yakuridhisha, hatuna budi kumruhusu kuondoka.”

Kwa sasa kikosi cha Simba SC kinasimamiwa na kocha msaidizi Denis Kitambi, na uongozi wa klabu hiyo umedhamiria kumtangaza kocha mkuu haraka iwezekanavyo, ili kuanza maandalizi rasmi ya kuelekea mchezo ujao wa ligi kuu dhidi ya Young Africans.

Simba SC watakua wenyeji wa Young Africans Januari 04 -2020 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam.

Video: Mbowe asafishiwa njia, PPRA yanusa ufisadi mabilioni taasisi 39
Faida ya Mbegu za maboga na jinsi inavyoshusha kiwango cha sukari

Comments

comments