Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kutangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma atakapozulu jimbo hilo Mei Mosi.

Rais Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) mwaka huu yatakayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.

Sugu amesema kuwa kwakuwa wafanyakazi hawajapandishiwa mishahara kwa kipindi cha miaka minne sasa, anamuomba Rais atoe tamko la kupandisha mishahara ili kuwaongezea ahueni ya maisha.

“Wafanyakazi wana hali mbaya sana katika maeneo yote ya nchi. Pia, [Rais] aangalie suala la wastaafu wapo wengi na wengine ni mwaka wa pili sasa hawajalipwa mafao yao,” Mbunge huyo alisema jana alipokuwa akitoa mchango wake Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Aidha, Mbunge huyo alimuomba Rais kuliangalia pia suala la malipo ya wastaafu, akieleza kuwa wapo maafisa wa jeshi la magereza ambao walishastaafu lakini wamekosa fedha ya kuwasafirishia mizigo yao hivyo wameendelea kukaa kwenye nyumba za kambi ya makaazi ya askari magereza.

Aliiomba Serikali kuanza kuliandaa suala la nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi kama haikuwa kwenye ajenda zao za mwaka huu, ili Rais alibariki.

Mwaka jana, akihutubia katika maadhimisho ya Mei Mosi mkoani Iringa, Rais Magufuli alisema kuwa atakapotangaza kuongeza mishahara ataongeza kwa kiwango cha juu.

Sudan: Waandamanaji waligomea jeshi kuongoza nchi, wapambana
Jeshi la Sudan kuongoza nchi miaka miwili