Mwanzilishi wa lebo ya Death Row Records, Marion ‘Suge’ Knight amekutwa na hatia ya kuua (voluntary manslaughter), katika tukio la kumgonga na gari na kumsababishia kifo mtu mmoja pamoja na kujaribu kumuua mwingine.

Voluntary Manslaughter inatajwa kuwa ni kitendo cha mtu kutekeleza tukio la mauaji kutokana na hali ya kughafirishwa au wakati ambapo akili yake ilikuwa katika hali ya mvurugiko.

Suge Knight amekubali kutumikia kifungo cha miaka 28 jela, katika uamuzi uliotolewa jana mahakamani, lakini hukumu rasmi ya kifungo hicho cha miaka 28 itatolewa rasmi Oktoba 4 mwaka huu, kwa mujibu wa ABC News.

Gwiji huyo kwenye kiwanda cha muziki nchini Marekani alikamatwa na kufunguliwa mashtaka mwaka 2015, baada ya kubainika kuwa alitumia gari lake kumgonga Carter ambaye alikufa baadaye kufuatia majeraha makubwa aliyomsababishia; baadaye alimkimbiza na kumgonga Cle Sloan ambaye alipata majeraha makubwa lakini alipona.

Alikuwa anakabiliwa na kifungo cha maisha jela lakini baada ya kubainika kuwa alighafirishwa kabla ya kufanya tukio hilo na hivyo kutokuwa sawa kiakili, amepewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 28 jela.

Knight ana heshima ya historia ya kuwatoa kimuziki wasanii wengi wakubwa kama Dr Dre, Tupac Shakur na Snoop Doggy kupitia Death Row Records.

Matangazo ya uzazi wa mpango yasimamishwa rasmi nchini
Chameleone, mkewe wafunguka baada ya kupigana chini