Viongozi wa maandamano yanayoendelea nchini Sudan yaliyosababisha kuondolewa madarakani aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kwa miaka 30, Omar al-Bashir wametangaza kuvunja uhusiano na mawasiliano na Baraza la Usalama la Kijeshi.

Maelfu ya waandamanaji wamekusanyika nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo jijini Khartoum wakidai kuwa muda wowote watatangaza Serikali ya kiraia. Wamesema Baraza la Usalama la Kijeshi limejaa sura za utawala wa al-Bashir.

Jeshi la nchi hiyo liliuambia Umoja wa Afrika hivi karibuni kuwa limejipanga kuwaachia waandamanaji kuunda Serikali ya kiraia, lakini itakuwa na uwakilishi wa Baraza la Usalama la Kijeshi .

Ahadi ya viongozi wa maandamano hayo kutangaza majina nya viongozi wa Baraza la Kiraia litakaloitawala Sudan kwa kipindi cha mpito hadi uchaguzi wa kidemokrasia utakapofanyika imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara. Kwa mujibu wa Reuters imeripotiwa kuwa kuna hali ya mvutano kati ya makundi yanayounda vuguvugu hilo yanayotofautiana kuhusu nafasi za utawala na sera.

Hadi Jumapili ya Pasaka, Baraza la Usalama la Kijeshi limeonekana kupata uungwaji mkono hususan kwa nchi za Saudi Arabia na Falme za Kiarabu. Nchi hizo zimelipa baraza hilo msaada wa takribani $3 bilioni.

Baraza hilo lilimkamata al-Bashir baada ya kumuondoa madarakani kufuatia vuguvugu la maandamano kisha likamuweka kwenye kifungo cha ndani kabla ya kumhamishia kwenye gereza lenye ulinzi mkali zaidi jijini Khartoum.

Wiki iliyopita, vyombo vya usalama vilipekua nyumbani kwa al-Bashir na kukuta mabegi pamoja na magunia ya fedha taslimu zenye jumla ya thamani ya $130 milioni. Mwendesha mashtaka wa Serikali amesema kuwa watamhoji gerezani anaposhikiliwa ili wamfungulie kesi ya utakatishaji fedha.

Arusha: Asimulia alivyohama ghafla kwenye gari iliyopata ajali, RPC azungumza
Sri Lanka: Idadi ya waliouawa kanisani, hotelini Pasaka yafikia mamia