Saa chache baada ya jeshi la Sudan kutangaza kuwa litaongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili baada ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Omar Al Bashir kung’olewa, waandamanaji wamejitokeza kwa wingi mitaani kupinga tangazo hilo.

Al-Bashir aliandamwa na waandamanaji hao waliokuwa wakipinga hali ya ugumu wa maisha, na jana jeshi la nchi hiyo lilimuondoa madarakani na kumkamata, na hivyo kuhitimisha utawala wake wa kipindi cha miaka 30.

Waandamanaji hao jana walikesha kwenye mitaa ya jiji la Khartoum, kinyume cha tangazo la jeshi la nchi hiyo lililomtaka kila raia kubaki ndani hadi hapo watakapotangaziwa tena.

Watu hao walioingia barabarani wanadai kuwa Baraza la Kijeshi lililochukua hatamu ni sehemu  ya utawala wa Al-Bashir.

Waziri wa Ulinzi, Ahmed Awad Ibn Auf alitangaza kuongoza Baraza la Kijeshi, lakini ni mmoja kati ya watu wanaokabiliwa na vikwazo vya Marekani.

Waziri wa Ulinzi, Ahmed Awad Ibn Auf

Hali hiyo imezua taharuki na hofu ya kutokea mapambano kati ya jeshi la nchi hiyo na waandamanaji.

Kwa mujibu wa mhariri wa BBC, Will Ross aliyeko nchini humo, kuna hofu kuwa huenda vyombo vya ulinzi na majeshi ya nchi hiyo ambavyo vina misimamo tofauti kuhusu Al-Bashir vikageuziana silaha.

Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika wametoa wito wa kuwepo kwa hali ya utulivu nchini humo.

Al-Shabaab wateka madaktari bingwa wa Cuba
Sugu awasilisha maombi yake kwa JPM atakapokuwa Mbeya