Kocha mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa mwamuzi wa mchezo wao wa jana dhidi ya Toto Africans, alitakiwa kuahirisha mechi hiyo ndani ya dakika 20 za mwanzo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jijini Mwanza.

Azam FC iliweza kuambulia sare ya bao 1-1 kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika  Uwanja wa CCM Kirumba, ambapo mvua hiyo ilianza kunyesha dakika chache kabla ya mechi hiyo kuanza.

Akizungumza na mwandishi wetu, Hall alisema walikuwa na vita tatu ndani ya mchezo huo, ya kupambana na hali ya uwanja, waamuzi pamoja na wapinzani wao hao, jambo ambalo liliwafanya washindwe kuishinda vita hiyo kwa kuambulia sare.

“Ni matokeo mabaya kwa upande wetu, lakini kuna sababu kadhaa zimepelekea hayo kutokea  la kwanza ni sehemu ya kuchezea mpira (pitch), ingekuwa ni mimi mpira usingechezeka, kwangu mimi baada ya dakika 20 ningeahirisha mchezo huo hata kabla ya sisi kupata bao baada ya mistari ya chaki kutoonekana, nilisimama eneo hilo na kuona mwamuzi msaidizi akishindwa kuiona mistari hiyo, hata mwamuzi wa kati naye alishindwa lakini hawakulizingatia hilo, vilevile mpira ulishindwa kuenda chini pale ulipopigwa kutokana na maji kujaa,” alisema.

Hall alisema baada ya mpira kuendelea ulikuwa ni wa nguvu sawa na kudai kuwa kwa hali ile huwezi kupata mchezaji bora kwani mipango ya timu inashindwa kwenda vizuri, kwani mchezaji huanza kupambana na uwanja kabla ya kufikiria jambo jingine.

“Wachezaji wangu walishindwa kwenda mbele na mipira kabisa, Sure Boy alishindwa, Farid Mussa alishindwa, Messi (Ramadhan Singano) asingeweza kucheza kwenye hali hii kwani ilikuwa ni ya kupambana sana,” alisema.

Magufuli aahirisha shamrashamra za sikukuu ya Muungano, abadili matumizi ya fedha za sherehe
King Kibaden Kujiweka Pembeni Na Soka