Makocha na wachezaji wa kigeni wanaocheza katika klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara wameingizia Serikali Shilingi bilioni 1.7 Katika kipindi cha 2017/18.

Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashantu Kijaji ametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 4, 2020 wakati akijibu swali la mbunge wa Chemba, Juma Nkamia.

Awali mbunge huyo amehoji Serikali imekusanya kiasi gani cha kodi kutoka kwa makocha na wachezaji wa kigeni wanaofanya kazi nchini katika kipindi hicho.

Hata hivyo Nkamia amesema ulipaji kodi kwa kada hiyo hauna mpangilio maalumu na kuwa serikali inapoteza fedha nyingi.

Naibu Waziri amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004, Kifungu cha Saba (7), kila mtu anayepata mapato yatokanayo na ajira ndani ya Tanzania anawajibika kulipa kodi ya mapato kulingana na kipato chake.

Amesema suala kujua nani anastahili kulipa kodi ni jukumu la mwajiri ambaye ndiye anatakiwa kutoa taarifa ana wafanyakazi wangapi na wanatakiwa kulipa kodi kiasi gani.

Dk Kijaji amesema serikali itaendelea kuwabana wafanyakazi na wachezaji wote ili walipe kodi stahiki na serikali iweze kupata mapato yake.

Membe kuhojiwa na Kamati ya CCM kesho, mwenyewe afunguka alivyojipanga
La Liga wataja muda wa kuanza kwa El Classico mzunguuko wa pili